15 December 2011

Yanga wajifua pekupeku

 Na Zahoro Mlanzi

*Waimba na kucheza Prakatatumba

MASHABIKI wachache wa Yanga, waliojitokeza Uwanja wa Shule ya Loyola, Dar es Salaam jana kuangalia mazoezi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara,
walipigwa na butwaa kutokana na wachezaji wa timu hiyo kufanya mazoezi bila viatu (pekupeku).

Pamoja na hali hiyo, kiungo wa timu ya taifa (Taifa Stars) na timu hiyo, Nurdin Bakari aliyekuwa majeruhi tangu yamalizike mashindano ya Kombe la Chalenji naye alianza mazoezi na wenzake.

Gazeti hili lilifika katika viwanja hivyo na kukuta wachezaji wameshaanza mazoezi, ambao walikuwa chini ya Kocha Mkuu Mserbia Kostadin Papic, pamoja na Msaidizi wake, Frded Minziro ambao walikuwa wakipiga mipira kulenga goli na mengineyo.

Lakini hali ndani ya uwanja huo, ilikuwa tofauti na vile ambavyo mashabiki walivyotarajia kwani uongozi wa timu hiyo, umekataza mashabiki na hata waandishi wa habari kuingia uwanjani kuangalia mazoezi yao kutokana na Papic kuomba hivyo.

Mwandishi wa gazeti hili alifanya jitihada binafsi na kufanikiwa kuwepo karibu na wanapofanyia mazoezi na kushuhudia zikiwa zimebaki dakika 15 kabla ya mazoezi kumalizika.

Wachezaji hao walifanya mazoezi kwa kuzunguka uwanja, huku wakiwa hawana viatu.

Hali hiyo iliwashangaza mashabiki wengi waliokuwepo nje ya uwanja huo, ambao walikuwa wakiangalia kupitia kwenye matundu ya uzio wa shule hiyo, huku wengine wakiwa wapo juu ya miti na kuwafanya kila mmoja kuzungumza lake.

Baada ya kuzunguka uwanja kwa raundi kama 10, huku wakiimba wimbo wa Cabo Snoop kutoka Angola wa Prakatatumba kwa sauti ya juu.

Baada ya hapo Papic, aliwaamuru kuacha zoezi hilo na badala yake kunyoosha misuli kwa kumalizia mazoezi. Baada ya kumaliza mazoezi kila mchezaji alivaa viatu vyake.

Kabla ya suala hilo kujitokeza, walinzi wa shule hiyo walizuia gari la waandishi kuingia ndani lakini, baada ya kujitambulisha waliruhusu kwa sharti la kutokwenda kuangalia mazoezi, kwani wamekatazwa kuruhusu mashabiki na waandishi kuingia.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu kuzungumzia hali hiyo, alisema ni kweli uongozi umeamua kutoruhusu waandishi na mashabiki kuangalia mazoezi baada ya kocha, Papic kuomba kwa sasa wafanye mazoezi kwa staili hiyo.

“Ni kweli ulivyoambiwa na mlinzi, uongozi umekataa na ndiyo maana tuliamua kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, Masaki na sasa tupo hapo ni utaratibu ambao tumejiwekea kwa sasa, ila baadaye tutaruhusu kama kawaida,” alisema Sendeu.

No comments:

Post a Comment