Na Zahoro Mlanzi
UONGOZI wa Klabu ya Simba, umetinga Idara ya Uhamiaji kushughulikia suala la kibali cha kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic ili aendelee kuinoa timu hiyo.
Idara hiyo ilimpa kibali maalumu, kocha huyo cha kufanyia kazi lakini baada ya kuona muda unakwenda bila kupata kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini ilimzuia kufanya kazi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema jukumu la kumuombea kibali Milovan, si la kwao ila wanachofanya ni kuwasilisha vyeti TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), baada ya kuvihakiki ndiyo wanawapa barua ya kwenda Uhamiaji.
“Jukumu letu lilikuwa ni kuwasilisha vyeti vya Milovan, TFF na hilo tumeshalifanya sasa wao (TFF) inabidi watuandikie barua sisi Simba na ndipo tutaichukua na kuipeleka Uhamiaji kitu ambacho TFF, wameshafanya na muda wowote kuanzia leo (jana) tunaipeleka barua hiyo,” alisema Rage.
Aliongeza kuwa kocha huyo yupo nchini kutokana na idara hiyo kumpa kibali cha muda tangu alipowasili.
Katika hatua nyingine, Rage alisema kocha huyo hajaanza kazi rasmi, kwani wanachosubiri ni Uhamijaji kumpa kibali ndipo atakapoanza kazi rasmi.
Hata hivyo kocha huyo juzi, alikuwepo katika mazoezi ya timu hiyo, ambayo yalianza juzi katika Uwanja wa Tanganyika Perkars.
Rage alisema kocha huyo ataanza kwa mazoezi magumu, ya kati na kisha ya kawaida na baada ya hapo ataomba mechi za kimataifa, ili aweze kuwajua vizuri wachezaji wake.
No comments:
Post a Comment