15 December 2011

Mpango wa kusindika taka Dar yaiva

Na Zena Mohamed

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam Dkt.Didas Massaburi amefungua semina ya mradi wa kupunguza taka katika jiji la Dar es Salaam kwa kuzitumia kutengeneza gesi na kupata pesa ambao utaanza kutumika hivi karibuni.
Akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jiji hilo juzi, Dkt. Massaburi alisema mradi huo utaanza kutekelezwa muda wowote kuanzia sasa baada ya taratibu zote kukamilika.

Alisema Benki ya Dunia (WB) imekubali kudhamini mradi huo baada ya kuona jiji hilo kukabiliwa na aina nyingi ya taka huku uzalishaji wake ukiongezeka kwa kasi kila kukicha.

Alisema takwimu zinaoneyesha kuwa ongezekao la watu katika Jiji la Dar es salaam ni kubwa na kwamba kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu milioni nne huku ongezeko ikiwa ni asilimia 4.5 na kusababisha uzalishaji mkubwa wa taka kwa siku.

Meya huyo alitaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni kuwawezesha wadau kutambua uwezekano wa kupata fedha kupitia mradi huo kutokana na hewa ya kabonidayoksaidi inayotokana na mkaa.

Alisema katika mafunzo hayo wadau hao watajifunza kwa undani na kuuelewa athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na taka na madhara yake hivyo kusaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya nchi.

"Mradi huu utasaidia kudhibiti taka kwa kuzikusanya na kuwezesha kupunguza hewa ya kabonidayoksaidi kwa kupata fedha kwa ajili ya manunuzi ya gesi,"alisema.

Alisema ongezeko hilo linasababisha uzalishaji wa taka tani 2600 kwa siku na kwamba mategeo ni kuongezeka hadi kufikia tani 5000 kwa siku ifikapo mwaka 2015.

Alisema pamoja na mambo mengine mradi huo unalenga kupunguza umasikini kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo ya Millenia Tanzania.

No comments:

Post a Comment