15 December 2011

Wizara yasitisha biashara ya wanyamapori hai

Na Zena Mohamed

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesitisha biashara ya wanyamapori hai kuanzia Desemba 9, mwaka huu.Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa Wizara,
Bw. George Matiko, imesema Serikali imezuia ukamataji, uingizaji na usafirishaji wanyamapori hai isipokuwa wadudu.

Alisema kutokana na tangazo la Serikali ambalo limetolewa Desemba 9, mwaka huu, wafanyabiashara wenye vibali halali vya kumiliki na kusafirisha wanyamapori ambavyo hadi Agosti 18, mwaka huu vilikuwa havijamaliza muda wake, kisheria walipaswa kusafirisha wanyama hao ndani ya siku 90.

“Tangazo hili limetolewa kwa kutambua kuwa, wakati amri ya kusitisha biashara ya wanyamapori hai ilipotolewa, kuna baadhi ya kampuni ambazo tayari zilikuwa na wanyamapori katika mazizi yao ambao walikamatwa kwa mujibu wa sheria.

“Muda uliotolewa kwa wafanyabiashara ni kwa mujibu wa kanuni za ukamataji wanyamapori za mwaka 2010, kanuni ya 12(4) na (5), inaelekeza kuwa wanyamapori waliokamatwa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi kibiashara walitakiwa kusafirishwa katika kipindi cha miezi mitatu tangu kukamatwa,” alisema.

Alisema matumizi mengine ya wanyamapori hai na mazao yake kwa shughuli zisizo za kibiashara na zenye manufaa kwa Taifa kama utafiti, yanaruhusiwa.

No comments:

Post a Comment