15 December 2011

Wanaomiliki silaha isivyo halali sasa kusakwa-Polisi

Na Mwandishi Wetu

JESHI la Polisi nchini lipo mbioni kufanya operesheni maalumu nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola na raia wema ili kuwabaini watu wanaomiliki silaha kinyume na taratibu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Bi.Advera Senso, aliyasema hayo Dar es Salaam jana, katika majumuisho ya kampeni ya usalimishaji silaha iliyoendeshwa na jeshi hilo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Agosti mosi hadi Oktoba 31, mwaka huu.

Alisema jeshi hilo lilizindua kampeni ya kuhamasisha jamii kutii sheria bila kushurutishwa kwa kuchukua hatua kadhaa ambazo zilikusudia kuondoa mianya inayoweza kusababisha matumizi mabaya ya silaha zinazomilikiwa kihalali au isivyo halali.

“Jeshi la Polisi lilitoa muda wa miezi mitatu kwa watu au mtu yeyote anayemiliki silaha kinyume cha sheria, kuisalimisha kwa hiari yake katika kituo chochote cha polisi au mamlaka za Serikali zinazohusika.

“Katika kipindi hiki, hakuna hatua zozote za kisheria zilizokuwa zikichukuliwa dhidi ya mtu aliyesalimisha silaha ambapo wamiliki halali, walitakiwa kufika Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya kwa ajili ya kuhakiki upya silaha zao,” alisema Bi.Senso.

Aliongeza kuwa, katika kipindi hicho silaha 59 zilisalimishwa, mabomu mawili ya kurusha kwa mkono na risasi 4,000 ambapo silaha 21,427, zilizohakikiwa upya katika maeneo mbalimbali.

Bi.Senso alisema miongoni mwa silaha zilizosalimishwa ni pamoja na shortgun (11), G3 moja, gobore (35), SMG nane, riffle mbili, pisto moja na SR moja.

“Operesheni hii imelenga kuwabaini wale wote wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu pamoja na wale waliokaidi kuhakiki silaha wanazomiliki kihalali ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema.

Alitoa wito kwa watu mbalimbali kuendelea kusalimisha silaha zao vituoni au katika mamlaka za Serikali zilizo karibu yao ambapo kazi ya kuweka alama maalumu ya utambuzi wa silaha zinazomilikiwa kihalali inaendelea.

“Tunatoa wito kwa wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa za mtu au kikundi cha watu wanaosadikiwa kujihusisha na umiliki wa silaha isivyo halali au matukio ya uhalifu wa aina yoyote,” alisema Bi.Senso.

No comments:

Post a Comment