07 December 2011

Vijana mkijitambua tutakomesha mimba za utotoni-Makinda

Salim Nyomolelo

SPIKA wa Bunge la Tanzania Bi. Anne Makinda, amekemea mimba za utotoni na kuwataka vijana kujitambua ili waweze kutimiza malengo yao na kukomesha vitendo hivyo.

Spika Makinda alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizindua ripoti ya usawa wa kijinsia ya kuwawezesha wanawake iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa Tanzania (UN) Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF).

Alisema takwimu za kina zilizofanywa na UNICEF zinaonesha kuwa Tanzania ina vijana wenye umri kati ya miaka 10-19 milioni 9.9 sawa na asilimia 23 ambao wanatakiwa kukua katika mazingira mazuri pamoja na kupata elimu bora.

Alisema idadi ya wasichana wanaopata mimba kati ya umri wa miaka 15 hadi 19 ilipungua kwa asilimia 12 kutoka wasichana 132 kwa kila 1,000 mwaka 2004 hadi kufikia wasichana 116 kati ya 1,000 kwa mwaka 2010.

"Kupungua kwa mimba za utotoni kunadhihirika katika kila kundi la kijamii kuwa na uchumi kwa mikoa yote," alisema Bi.Makinda

Alisema pamoja na mafanikio hayo Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo zina idadi kubwa ya mimba za utotoni na uzazi na kwamba tafiti za kina zinaonesha msichana mmoja kati ya sita wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ameolewa huku mmoja kati ya 10 anakuwa na mtoto anapofikisha umri wa miaka 16.

Alisema tafiti hizo zilionesha kuwa asilimia 8.5 ya watoto waliozaliwa na wanawake wenye umri kati ya miaka 20 kutoka familia maskini walikuwa na uzito chini ya kilo 2.5 ikilinganishwa na asilimia 6.7 ya watoto waliozaliwa na wanaotoka katika familia tajiri.

Alisema mimba za utotoni zinasababisha madhara makubwa ikiwamo vifo huku watoto wakikosa mazingira mazuri kutokana na kuzaliwa na watoto wenzao.

No comments:

Post a Comment