07 December 2011

Mchungaji apigwa radi shambani

Na Esther Macha, Mbeya

MCHUNGAJI wa Kanisa la House Of Prayer Seleman Liduke (51) katika Kijiji cha Kapunga, Kata ya Mapogoro Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya amefariki dunia
baada ya kupigwa na radi akiwa shambani kwake.

Tukio la Mchungaji huyo kupigwa na radi lilitokea saa 12 jioni Desemba 5 mwaka huu katika Kitongoji cha Kapunga Site One  wilayani humo.

Mchungaji huyo alipatwa na umauti akiwa shambani kwake baada ya kutoka katika banda ya kufukuzia ndege alilojihifadhi wakati mvua hiyo kubwa iliyoambatana na radi ikinyesha na kwamba baada ya kumalizika alitoka katika banda hilo na ghafla ilitokea tena ngurumo iliyoambatana na radi.

Mchungaji huyo alipoteza maisha papo hapo baada ya kupigwa radi usoni na kusababisha kuvunja damu mdomoni na puani huku nguo zake zikiwa zimeshika moto.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mtoto wa marehemu Bw. Boaz Liduke (16), ambaye pia ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kapunga, alisema alipoona baba yake amechelewa kurudi alimfuatilia hadi shambani ndipo alipomkuta  amefariki nje ya kibanda cha kuamia ndege.

Alisema baada ya kubaini kifo cha baba yake alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji cha Kapunga Site one ambao walitoa taarifa haraka kituo cha Polisi Chimala.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji hicho Bw. Ibrahimu Mwandungu, alisema baada ya kupata taarifa katika kituo hicho polisi walifika eneo la tukio na kuthibitisha kifo hicho kilichotokea umbali wa kilometa moja toka nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Bw.Advocate Nyombi, alisema taarifa hizo bado hazijamfikia rasmi na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.

No comments:

Post a Comment