06 December 2011

Utekelezaji mafunzo ya JKT kisheria waanza

Na Rabia Bakari

 WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, amezindua jengo la Chuo cha Mafunzo kwa Wakufunzi wa Jeshi hilo katika kambi ya Kimbiji Jijini
Dar es Salaam kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali kurejesha mafunzo ya JKT nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana, Dkt. Mwinyi, alisema chuo hicho kitaandaa maofisa na maaskari wa jeshi katika nyanja tofauti na kwamba huo ni mwanzo wa ujenzi wa vyuo vingine kadhaa vya mafunzo nchini.

"Serikali ipo katika mchakato wa kurudisha mafunzo ya JKT kwa vijana kwa mujibu wa sheria, chuo hiki ni moja ya mikakati ya kuwaandaa wakufunzi kusimamia vizuri mwongozo wa malezi ya vijana wa sasa,"alisema Dkt. Mwinyi.

Naye Mkuu wa JKT Meja Jenerali Samwel Kitundu, alisema awali chuo hicho kilipangwa kujengwa eneo la Jeshi hilo Mbweni lakini Rais Jakaya Kikwete, alitoa maelekezo kutafuta eneo lingine ili Mbweni libaki kwa ajili ya shughuli za kitalii.

Alisema jengo hilo limejengwa na wataalamu kutokana ndani ya Suma JKT hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingelipwa kwa wakandarasi na watalaam kutoka nje.

Alisema baada ya vyuo mbalimbali vya uongozi kufungwa miaka ya nyuma hawakuwa na sehemu ya kuwaandaa wakufunzi wa JKT na kwamba waliokuwepo walistaafu huku ikikosekana maandalizi kutayarisha wengine wapya.

Meneja Mradi wa ujenzi wa chuo hicho Mhandisi Peter Ngata, alisema ujenzi huo ulianza Julai 20 mwaka huu na ulitarajiwa kukamilika katika wiki 22 lakini  wafanikiwa kumaliza wiki kabla ya muda wa makadirio licha ya changamoto mbalimbali walizokutana nazo.

"Pamoja na kukamilika kwa jengo hili, ujenzi huu ni endelevu bado kuna majengo kadhaa yaliyopangwa kujengwa ikiwemo nyumba za wafanyakazi, shule, zahanati, na majengo ya makazi kwa ajili ya wanafunzi,"alisema.

No comments:

Post a Comment