13 December 2011

Ubalozi wa Israel utaleta baraka kwa TZ-Askofu

Na Rabia Bakari

SERIKALI imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kufungua haraka Ubalozi wa Israel nchini kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya kwa kuwa  taifa hilo lina ahadi za baraka za
Mungu zenye manufaa ya maendeleo.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Jimbo la Mashariki, Mchungaji Lawrence Kametta, katika mkesha wa kuiombea taifa uliofanyika katika kituo cha Amani Dar es Salaam.

“Uhusiano kati ya Tanzania na Israel ukirudi utazaa matunda na mfano mzuri ni Kenya ambayo  inaongoza kwa mambo mengi katika Afrika Mashariki, moja ya siri yake ni kutokana na kuwa na uhusiano kwa kibalozi na Israel.

"Matokeo ya uhusiano huo hata Mlima Kilimanjaro upo hapa nchini lakini fedha za utalii zinaingia Kenya, mbuga za wanyama nyingi zipo fedha zake zinaingia Kenya, Tanzanite ipo nchini lakini wauzaji wakubwa duniani wa madini hayo wapo nchini Kenya,”alisema Askofu Kametta.

Askofu huyo aliishauri pia serikali kuwa na uongozi wa kizalendo usioegemea dini moja wala kupendelea watu wa kada fulani na kutatua kero za muungano.
 
Aliitaka serikali kuweka uwiano mzuri wa kupata huduma za msingi unaotokana na mapato ya utajiri wa taifa kati ya wageni na wazawa.

“Tanzania ina rasilimali nyingi na za kutosha ambazo zinatakiwa kuwepo na uwiano wa kuzitumia rasilimali hizo kati ya wawekezaji wageni na wazawa ili mali hiyo iweze kumnufaisha kila mmoja wetu kwa manufaa ya taifa,”alisema Askafu Kametta.

Askofu Kametta aliongoza maombi maalum  kuhakikisha miaka 50 ijayo nchi inakuwa makini katika mahusiano yake na nchi za nje na kwamba wananchi wawe wameandaliwa vya kutosha kuingia katika mahusianao na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Maombi mengine yahusu viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Rais Jakaya Kikwete, kwa kuifikisha nchi katika miaka 50 kwa amani.

“Uhuru wa kuabudu uheshimiwe na pande zote bila upendeleo wowote, ni vyema kuangalia  mambo mawili ikiwa ni pamoja na kuvumiliana na kuheshimiana.

Katika hatua nyingine Mchungaji Kametta alikabidhi vyeti kwa wachungaji 43 ambao walianza safari juzi kuelekea mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, kwa ajili ya kutangaza amani na neno la mungu.

No comments:

Post a Comment