07 December 2011

Twanga yarejea na mikakati

BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta'
imewasili Dar es Salaam jana ikitokea London,
Uingereza na kuweka mikakati yake ya kuimarisha soko la kimataifa na la hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa bendi hiyo, Luizer Mbutu alipokuwa anazungumzia mafanikio na changamoto za maonesho yao, yaliyofanyika nchini Uingereza.

Luizer alisema wamepata mafanikio makubwa katika maonesho hayo ya wiki mbili, huku moja likiwa la kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Alisema tofauti na ziara yao ya kwanza ya mwaka 2005, safari hii walikwenda kufanya shoo huku wakizinadi CD na DVD za albamu zao za nyuma, zikiwa katika maonesho ya ‘live’ na ya kawaida ambazo walifanikiwa kuziuza zote.

“Kwa kweli tumefarijika mno na maonesho na kufanikiwa kuuza kazi zetu nchini Uingereza, kazi iliyobakia sasa ni kuimarisha soko hilo, huku tukifanya kazi kama hiyo hiyo hapa nyumbani,” alisema Luizer.

Alisema maonesho yao yalijaza watu mbalimbali wa mataifa tofauti na kupata mwaliko mwingine, ambao uongozi utaamua lini watarejea huko.

“Naupongeza uongozi wa ASET chini ya Mwenyekiti, Msilwa na Mkurugenzi, Asha Baraka kwa kufanikisha ziara hii ya tatu kwa bendi kufanya maonesho Ulaya, mwaka 2005 tuliweza kufanya maonesho katika nchi tano za Scandinavia na mwaka uliofuata tukaingia London kwa mara ya kwanza,” alisema.

Alisema hawakuwa wanakaa tu kusubiri kazi za kufanya maonesho, kwani wameweza kutunga nyimbo mbili, mmoja unajulikana kwa jina la Back to London uliotungwa na Chalz Baba na Uzuri wa mwanamke si tabia bali ulivyopendezewa, uliotungwa na Saleh Kupaza.

Kiongozi huyo alisema nyimbo hizo zitafanyiwa mazoezi, ili kuziimarisha na kuanza kupigwa katika maonesho yao mbalimbali ya mwisho wa wiki hii.

Naye Asha, aliwapongeza wote waliofanikisha ziara hiyo na kusema kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya maonesho ya hapa nchini na ziara nyingine za nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment