06 December 2011

Wazazi CCM Watoa tamko

Na Anneth Kagenda

*Yawataka Watanzania kukataa uporwaji rasilimali
*Yasisitiza umuhimu wa madini kunufaisha wazawa
*Zungu: Unyonywaji sasa basi, katiba mpya iamue

MBUNGE wa Jimbo la Ilala, Dar es Salaam, Bw.Azzan Zungu,
amewataka Watanzania kuonesha kwa vitendo jinsi walivyochoshwa kuibiwa na kunyonywa rasilimali zao na wawekezaji.

Bw.Zungu aliyasema hayo Dar es Salaam juzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari walioshiriki katika uzinduzi wa semina ya Jumuiya ya Wazazi, wilayani Kinondoni.

Lengo la semina hiyo lilikuwa kutoa elimu kwa jumuiya hiyo kuhusu sheria ya mchakato wa Katiba Mpya ili waweze kujua wajibu wao baada ya tume maalumu kuanza kukusanya maoni.

Alisema wananchi wanapaswa kushinikiza uwekwaji kipengele ambacho kitaitaka nchi kubaki na asilimia kubwa ya mapato yatokanayo na madini katika rasimu ya Katiba Mpya na kukataa asilimia tatu ya sasa wakati wageni wakiondoka na asilimia 97.

Semina hiyo ililenga kutoa elimu kwa wana CCM kuhusu sheria ya mchakato wa Katiba Mpya ili kuwawezesha kujua wajibu wao muda wa kutoa maoni utakapowadia.

“Napenda kusema kuwa, ni wakati muafaka kwa Watanzania kuhakikisha wananufaika na uwekezaji kwa kupata asilimia kubwa na wageni kupata kidogo, suala la kuwaneemesha wawekezaji limepitwa na wakati.

“Watanzania waamue nini cha kufanya katika nchi yao kwa mfano nchi ya Canada, mwekezaji anachukua asilimia 38 zinazobaki zinakwenda kwa wazawa, tuseme tumechoka,” alisema Bw.Zungu.

Aliongeza kuwa, wawekezaji wanakuja nchini na kujichotea rasilimali zilizopo wanavyotaka hivyo jambo hilo linapaswa kukoma katika kuelekea miaka 50 ijayo ili Watanzania wapate maendeleo makubwa.

“Ikumbukwe kuwa tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa kuna Watanzania ambao wanashiriki katika uwekezaji lakini si rahisi kwa jamii kubwa kufahamu hili, wapo wawekezaji kutoka ndani ya nchi tuangalie suala la wawekezaji wa nje kuchota rasilimali zetu na kwenda kujinufaisha, tuseme kwa kauli moja sasa basi,”alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuia hiyo Taifa, Balozi Athuman Mhina, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo, aliwashauri Watanzania kuwa mstari wa mbele kushiriki katika mchakato wakuandaa Katiba Mpya.

Alisema katika kuelekea miaka 50 ijayo, wazazi hawana budi kufundisha maadili mema katika jamii ili kupata viongozi bora wa kuongoza Taifa la kesho.

“Hivi sasa maadili yamemong'onyoka sana, hali hii inachangiwa na sababu kubwa moja, zamani mtoto wa mwenzako ungeweza kumchapa lakini hivi sasa huwezi kufanya hivyo, jambo hili linachangia kuzalisha viongozi wabovu,” alisema.

Alisema CCM imejipanga vizuri katika mambo mbalimbali likiwemo kuwaengua wanachama na viongozi waliosababisha chama hicho kikose ushindi katika majimbo ya Kawe na Ubungo, Dar es Salaam ambapo viongozi hao wanajulikana.

“Jumuia ya Wazazi tunaahidi kuwatosa wote waliosababisha majimbo haya kwenda upinzani, hawa viongozi wanafanya mambo kwa chuki binafsi ili chama kiweze kuanguka.

“Hatuwezi kukaa na watu wanaokigawa chama, leo wako huku kesho wako kule, lazima tujipange sawa sawa kuhakikisha tunawatosa na kusonga mbele zaidi,” alisema Balozi Mhina.

Akizungumzia mazungumzo kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Rais Jakaya Kikwete, Balozi Mhina alionesha kushangazwa na chama hicho kumfuata kiongozi wao Ikulu wakati walitamka kutomtambua baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010.

“Mimi nadhani hawa CHADEMA walitaka kuiona Ikulu inafananaje ndio maana wakaomba kuzungumza na Rais Kikwete, tunawaambia kwamba, rais wetu anakubalika hata vyama vingine wakitaka wanaruhusiwa, kiongozi wetu hana matatizo yoyote,” alisema.

Akifunga semina hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Bw.Ramadhani Madabiba, alisema wakati nchi inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 56 ya Jumuiya ya Wazazi, Serikali ya chama hicho imefanya mambo makubwa hivyo inastahili pongezi.

Katika semina hiyo, maazimio 13 yalipitishwa ikiwemo kutoa elimu kwa wana CCM wote kuhusu sheria ya mchakato wa Katiba pamoja na kumpongeza Rais Kikwete kwa uvumilivu na usikivu wake ambao umesaidia kukuza demokrasia.

Maazimio mengine ni jumuiya hiyo kushirikiana na Serikali kupambana na mmomonyoko wa maadili hasa matumizi ya dawa za kulevya, kupiga vita biashara ya ukahaba, kuhakikisha uchaguzi mkuu wa chama na jumuiya unakuwa huru na haki na kutoruhusu mamluki kutumia fedha ili kununua viongozi na kuwatosa wote waliokihujumu chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Serikali za Mitaa, Madiwani na Wabunge kuanzia mwaka 2009/2010.

4 comments:

  1. Huyo Mhina kama si mnafiki mkubwa kwanini hakuyasema hayo kabla Chadema hawajaenda Ikulu. Upuuzi mtupu. Hebu atupe maoni yake pia kuhusu Matamshi ya Lowasa katika kikao cha mwisho cha CCM kule Dodoma, ndipo tujue yuko wapi kimtazamo.

    ReplyDelete
  2. hao wote ni bendera fata upepo,raisi wao angekua anakubalika angepata kura 5milion?wanaogopa kuvua gamba litatoka na nyama.

    ReplyDelete
  3. Mheshimiwa Zungu, mbona hatujakusikia ukizungumza hayo kwenye vikao vya Bunge. Huzungumzii fedha zinavyotafunwa Mali Asili, Wawekezaji wanaposhirikiana na viongozi wa Chama na Serikali kukwapua fedha mali za Watanzania . hatujasikia umetishia kuondoa shilingi bungeni. Usituhadae sisi wana kinondoni na watanzania. Jumuiya ya Wazazi haitatusaidia. Kazi kula fedha zinazochangwa na Wazazi na Serikali yetu. Mhina anaweza kuwapa wanachama wake na watanzania mapato na Matumizi ya Umoja huwake. atasema ni siri. Kaani tu mlle vya watanzania mkidhania bado ni mbumbumbu Ache kutupa porojo . Siku yenu ya arobaini itawafikieni.

    ReplyDelete
  4. Huyo Mhina ni mpumbafu kweli. Hivi hii ndio aina ya viongozi wa CCM kweli. Hivi kweli mnampa mtu kama huyu uongozi mnategemea nini? Rais wao na nani? Hivi Kikwete ni rais wa Tanzania au ni rais wa CCM? Huu ujinga jamani hata waandishi wakati mwingine muwe mnaangalia na cha kuandika. Au pengine meandika ili tuone upande mwingine wa viongozi wa CCM makanjanja. Kuhusu Zungu anachoongea, ni afadhali anawaeleleza huo umoja wa wazazi wa CCM. Huu uppuzi anauongelea hapa angefanya kikao cha wanajimbo na kueleza haya tungempa kichapo kama Kibaka. Alikuwa wapi kueleza bungeni? Hivi viongozi wa juu wa CCM na serikali yake hivi hawaelewi uhuhumu wa raslimali kuwanufaisha watanzania? Ama kweli najuta kuishi hii karne amabayo na kukutana na viongozi wa aina hii. Mnatupa bure shinikozo la damu.

    ReplyDelete