08 December 2011

Tamasha la kumkumbuka Remmy leo

Na Mwali Ibrahim

FAMILIA ya mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini ambaye kwa sasa ni marehemu Remmy Ongara, inatarajia kufanya tamasha la kumbukumbu yake litakalojulikana
kwa jina la 'Ubongo Festival'.

Tamasha hilo linatarajia kufanyika kesho katika viwanja vya Leders Kinondoni, Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo kutakuwa na burudani kutoka bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' Mrisho Mpoto na Excel one inayoimba nyimbo za nguli huyo.

Bendi nyingine zitakazotumbuiza ni Matimila Tribute, Fidd Q, Chidi benz, Msondo Music, Banana Zoro, Jikhoman, Kalora Kinasha, Kundi la Uhuru na msanii kutoka Uingereza Planetman.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mtoto wa mwanamuziki huyo Aziza Ongara, alisema tamasha hilo litakuwa likifanyika kila mwaka na mapato yatakayopatikana yatapelekwa katika kituo chao cha kulelea watoto cha Remmy Ongara Foundation.

Alisema kituo hicho cha Remmy licha ya kulea watoto yatima pia kitakuwa kikitoa elimu ya muziki kwa watoto wenye vipaji vya muziki, wanaolelewa na kituoni hapo.

"Tutakuwa tukitafuta watoto wenye vipaji vya muziki kutoka mikoani, mitaani na katika nyumba za kulelea watoto yatima, kwa sasa tutaanza na watoto 20 tutakaowapa mafunzo katika kituo chetu Sinza kwa Remmy," alisema Aziza.

Aziza alisema lengo la kufanya hayo ni kwa ajili ya kumuenzi mwanamuziki huyo, pamoja na kuthamini kazi zake kwa kuwa alikuwa akitunga nyimbo zenye kuienzi jamii na hata kueleza jambo kwa wakati husika.

Katika kuendelea kuenzi kazi zake, familia hiyo ipo katika mchakato wa kutemgeneza remix ya nyimbo zote, alizoziimba mwanamuziki huyo kwa kushirikiana na wanamuziki mbalimbali.

Naye Mpoto alisema kutokana na kuthamini mchango wa Remmy katika kumsaidia kuinuka kimuziki, anatarajia kutunga wimbo maalumu kama zawadi kwa mwanamuziki huyo na familia yake.

No comments:

Post a Comment