Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Castle Lite, jana imetangaza udhamini wa mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu yatakayofanyika Dar es Salaam, kuanzia
tarehe Jumapili hadi Desemba 17 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa Castle Lite, Pamela Kikuli alisema udhamini huo utagharimu sh. milioni 28.
"Tuna imani fedha hizi zitatumika vyema katika maeneo yaliyokusudiwa, ili kuleta tija katika mchezo huu wa mpira wa kikapu, tutaendelea kuwa mstari wa mbele kuuendeleza mchezo huu hapa nchini.
Pamela alisema wamefurahi kupata nafasi hii ya kudhamini mashindano haya muhimu, ambayo watashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), kuhakikisha yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Alisema mpira wa kikapu umekuwa na mvuto mkubwa na kuendelea kujizolea mashabiki wengi hapa nchini na duniani kwa ujumla.
Pamela alisema zaidi ya kuwa chanzo kizuri cha ajira kwa vijana, mpira wa kikapu pia unatoa fursa kwa washiriki kufanya mazoezi ya kutosha na hivyo kuwa na afya bora wakati wote,” alisema.
Naye Meneja Mahusiano na Habari wa Kamapuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo ndiyo huzalisha bia Castle Lager, Edith Mushi alisema mashindano ya mwaka huu yatashirikisha mikoa 18.
Aliitaja mikoa itakayoshiriki kuwa ni Ilala, Pemba, Tabora, Manyara, Kinondoni, Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Temeke, Tanga, Iringa, Arusha, Unguja, Mara, Rukwa, Lindi, Shinyanga na mbeya.
Alisema mashindano hayo yatashirikisha timu za wanaume na wanawake na yanatarajia kuwa na msisimko mkubwa miongoni kwa wanamichezo kote nchini.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa TBF, Mike Maluwe aliishukura TBL kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa kudhamini mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment