08 December 2011

TWFA yapata Mwenyekiti mpya

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Mpira wa Miguu cha  wanawake Tanzania (TWFA), Mkoa wa Pwani kimepata Mwenyekiti mpya na Wajumbe katika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hizo, baada ya
nafasi hizo kuwa wazi kwa kipindi kirefu.

Uchaguzi huo ulifanyika kwenye Ofisi za Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), ambapo Isege Mabula alichaguliwa kuwa Mwenyekiti.

Nafasi ya Katibu Msaidizi ilinyakuliwa na Saumu Muya, aliyekuwa mgombea pekee.

Katika nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Lydia Masena alipita baada ya kumshinda Magdalena Mwinuka.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, Isege aliwashukuru wajumbe waliomchagua na kusema kwamba atatoa ushirikiano kwa wadau wote wa mchezo huo ili kufanya soka la wanawake Pwani, liweze kukua.

“Kwa muda mrefu nafasi tulizojaza leo zilikuwa wazi, hali iliyosababisha ufanisi katika utendaji kazi kuwa chini, lakini mara baada ya uchaguzi huu tatupata fursa ya kufanya kazi vizuri na kila mtu atawajibika kwa nafasi yake,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho, Florence Ambonisye alisema walilazimika kuziba nafasi hizo zilizoachwa na viongozi hao, ambao wameshindwa kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali hali iliyokuwa ikiwafanya washindwe kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi za kila siku.

Florence alisema hata hivyo wajumbe 9 kutoka Wilaya za Mafia, Rufiji na Mkuranga hawakuweza.

No comments:

Post a Comment