14 December 2011

Simba kusherekea miaka 75 mwakani

Na Zahoro Mlanzi

UONGOZI wa Klabu ya Simba, unatarajia kufanya sherehe ya kuadhimisha miaka 75, tangu kuanzishwa kwake ambapo imepanga kucheza mechi za kirafiki za kimataifa na mambo mengine Januari 31, mwakani.

Mbali na hilo, pia klabu hiyo imepanga kupiga kambi Malawi mwakani, kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu Bara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema wamepanga kuadhimisha miaka hiyo kwa kukutana na wanachama wao wote Dar es Salaam, ambapo watafanya shughuli mbalimbali.

“Klabu yetu ilianzishwa 1936, tumeona si vibaya kama siku hiyo tukakutana pamoja na wanachama wetu, tukakumbushana mambo mbalimbali na kupanga miaka ijayo nini cha kufanya, ili timu yetu ipate mafanikio zaidi,” alisema Rage.

Alisema mara baada ya kumalizana na wanachama wao, watahakikisha wanapata mchezo mmoja wa kirafiki wa kimataifa, ili mashabiki wao wamalizie maadhimisho hayo kwa burudani ya aina hiyo.

Wakati huohuo, Rage alisema Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic tayari ameshawasilisha ripoti yake kwa ajili ya mashindano ya Ligi Kuu Bara na ya kimataifa, ambapo programu hiyo imeanza jana.

Alisema katika programu hiyo, Milovan amepanga kuanza na mazoezi magumu, yakifuata ya kati na karibu ligi kuanza atafanya mepesi, ili kuwaweka sawa wachezaji kwa mashindano yaliyo mbele yao.

Rage alisema pia amezungumza na Kocha Mkuu wa Malawi, Kinnah Phiri wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji, ambaye aliialika Simba waende wakapige kambi nchini humo na tayari suala hilo amemwachia Katibu Mkuu wa timu hiyo, Evodius Mtawala kulifuatilia.

“Kocha wetu Milovan ameonesha kuwa yupo makini sana, bila kuulizwa tayari ameshaleta programu yake ya mazoezi huku akisisitiza kuhitaji mechi zaidi za kimataifa ili aweze kuwaona wachezaji wake,” alisema Rage.

No comments:

Post a Comment