*Asema imeshindwa kuwakamata wahujumu uchumi
*Amsihi JK kusikiliza maoni ya wapinzani Katiba Mpya
Na George Boniphace, Mwanza
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Farijika Familia kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Kanisa Katoliki, Padri Baptisti Mapunda, amesema Serikali ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewasaliti wananchi baada ya kushindwa kuwakamata na kuwachukulia hatua mafisadi wanaohujumu uchumi wa Taifa.
Alisema usaliti wa Serikali kwa wananchi unatokana na baadhi ya viongozi serikalini kupata nafasi hizo kwa mgongo wa mafisadi hivyo ni vigumu kuwakamata na kuwachukulia hatua hali ambayo inachangia umaskini wa Watanzania.
Padri Mapunda aliyasema hayo jana kwenye Ibada Maalumu ya kufunga kongamano ambalo liliandaliwa na shirika katika Parokia ya Nyakato, Jijini Mwanza na kuongeza kuwa, Serikali ya CCM haina budi kubadilika na kuwachukulia hatua kali mafisadi kwa kuwa wanafahamika.
Alisema kitendo cha kuwakumbatia watu wanaotuhumiwa kuhujumu mali ya umma kwa njia mbalimbali ni kutowatendea haki wananchi pia ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Padri Mapunda, alimtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kuwa makini na suala hilo ili asije akalaumiwa baada ya kumaliza muda wake.
“Nchi yetu imefikia mahali pabaya, watawala wanatumia umaikini wa wananchi kuendesha nchi wanavyotaka, namuomba Rais Kikwete asipuuze maoni yanayotolewa na vyama vya upinzani kuhusu mchakato huu kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa, maoni ya wananchi yasipozingatiwa ni sawa na kuanzisha utawala wa kidikteta kinyume na utamaduni wa Mtanzania.
Alisema katika mchakato huo, viongozi wa dini wapewe nafasi ya kutosha ili watoe maoni yao kama ilivyofanyika nchini Kenya na kuepuka usiri katika suala hilo.
Alisema kuwepo kwa usiri katika mchakato huo kunaweza kuzua hofu ya kuibuka kwa utawala kandamizi, kukosekana uhuru wa kutoa maoni, kuabudu na kuamua jambo.
No comments:
Post a Comment