12 December 2011

Mbunge: Katiba iliyopo inakwamisha uwajibikaji

Na Joseph Mwambije, Songea

KATIBA iliyopo sasa, inawafanya wabunge washindwe kutekeleza wajibu wao kwa wapiga kura waliowapa madaraka na kuwageuza viongozi kuwa Miungu watu.Mbunge wa
Viti Maalumu mkoani Ruvuma kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Legia Mtema, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kongamano la katiba ambalo liliandaliwa na chama hicho.

Kongamano hilo lilishirikisha wanachama na viongozi 220 kutoka Wilaya zote mkoani humo ambapo Bi. Mtema na Katibu wa chama hicho Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, Bw. Powel Mfinanga,
walizungumzia Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya 2011, pamoja na kueleza sababu ya CHADEMA kuupinga.

Bi. Mtema alisema, chama hicho kimeandaa makongamano ya aina hiyo nchi nzima ili kueleza msimamo wa chama kupinga mchakato uliotumika kupitisha muswada huo.

Alisema wabunge wa chama hicho walikuwa sahihi kutoka bungeni kama hatua ya kuupinga muswada huo ambao mchakato wake haujashirikisha wananchi.

“Kamati Kuu ya CHADEMA inawaunga mkono wabunge wote ambao na kuwapongeza kwa kususia vikao vya Bunge ambavyovilijadili na kupitisha muswada huu,” alisema.

Alisema CCM inaamini kuwa, kupatikana kwa katiba mpya ambayo itatokana na matakwa ya Watanzania, upo uwezekano mkubwa wa chama hicho kuondolewa madarakani.

“Katiba tuliyonayo inampa Rais madaraka makubwa, urais wake unafananishwa na mfalme kutokana na katiba kupora haki ya wananchi ambapo mamlaka yamebaki kwa viongozi.

“Katiba hii inawafanya wabunge washindwe kuwajibika ipasavyo kwa wapiga kura waliowapa madaraka, uchaguzi ukiisha wananchi wanafungiwa vioo, wakati wa uchaguzi ukifika, wabunge wanahonga fedha ili wachaguliwe, katiba mpya wanayoitaka wananchi, itawafanya viongozi wawajibike ipasavyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika mchakato wa kupata katiba mpya kutakuwa na Bunge la Katiba lenye wajumbe 595 ambao wengi wao ni kutoka CCM na baadhi ya wajumbe wa kuteuliwa na Rais.

Bi. Mtema alisema hali hiyo ndiyo inawafanya waone kwamba, katiba mpya itakuwa ya CCM si ya Taifa hivyo msimamo wao ni kupata katiba ambayo itashirikisha wananchi wote vinginevyo watafanya maandamano nchi nzima ili kuipinga.

No comments:

Post a Comment