12 December 2011

CHADEMA:Tunachunguza za vigogo kuchimba madini

Na Bryceson Mathias, Mvomero

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro kimesema  kinafanyia kazi taarifa za wananchi kwamba kuna viongozi wamebadilisha
matumizi ya ardhi ya kilimo cha mpunga na miwa wami na kuanza kuchimba dhahabu kwa njia za panya.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Mvomero Bw. Dismas Ngeresha, alisema zipo taarifa zisizo rasmi kutoka kwa wananchi kwamba viongozi wanachimba dhahabu wami.

Alisema baada ya chama chake kupokea taarifa hizo wanazifanyia kazi kwa kina ili kujua ukweli wake na kwamba hawawezi kukurupuka kutoa tamko la kukubali au kukataa kwa kuwa mchakato wa kupata ukweli bado haujaka milika.

“Hatuwezi kuwataja waliotutonya kuhusu kuwepo uchimbaji huo kwa njia za panya, wananchi hao kwa sasa wanatusaidia kubaini ukweli wa mbichi na mbivu, interejensia yetu ikibaini  tutaijulisha Jamii,”alisema Bw.Ngeresha.

Diwani wa Kata ya Mtibwa aliye jirani na eneo linalotajwa kufanywa kwa uchumbaji huo Bi. Tusekile Mwakyoma, alipoulizwa alisema amesikia taarifa hizo na kwamba anafuatilia undani na kwamba iwapo zitathibitika chama chake kitajua cha kufanya.

Wakizungumza na mwandishi wa habari wananchi mbalimbali wa eneo hilo wakiwemo wafanyakazi wa shamba la miwa la wami Dakawa walidai kuwa taarifa hizo ni kweli na kuomba hatua za haraka zichukuliwe.

Mmoja wa wananchi hao Bw. Songa Mgweno, alisema kinachodaiwa kufanyiwa na viongozi hao kipo lakini kinafanywa kwa usiri mkubwa na kwamba udongo wenye madini unapakiwa kwenye magari usiku na kwenda kuchambuliwa mto wami.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero Bi. Sara Linuma,alipoulizwa suala hilo alisema haijamfikia rasmi na kwamba kwa kuwa ni la kijamii atalifuatilia.

No comments:

Post a Comment