Na Mwandishi Wetu
IKIWA imebaki wiki moja kabla ya pambano la bendi zenye upizani mkubwa nchini, Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park (Sikinde), tayari bendi hizo zimeamua
kupiga kambi kujiaanda na pambano hilo litalofanyika siku ya Krismas kwenye viwanja vya TCC Chang’ombe, Temeke.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana zimeeleza kwamba Msondo Ngoma, imeweka kambi yao jijini Mwanza wakati Sikinde, 'wamejificha' jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti, alisema wameamua kwenda mbali na Dar es Salaam ili kujiandaa vyema na mpambano huo.
“Litakuwa ni pambano kubwa na muhimu kwetu, inatulazimu tujiandae vyema ili tusije tukaangusha wapenzi wetu.
"Tumeamua kwenda Mwanza kwa sababu ni sehemu tulivu ya kujiandaa. Tukirudi Dar es Salaam kazi itakuwa moja tu, kuwashinda watani wetu,” alisema.
Naye Ofisa Mipango wa Sikinde Hamisi Mirambo, alisema wao watabaki jijini Dar es Salaam kwa kuwa wanajua wapinzani wao hawawatishi kwani watashusha burudani ya nguvu siku hiyo.
Sisi hatuendi mbali, tutajificha hapa hapa jijini kutayarisha nyimbo zetu mpya, ambazo tutazitumia kuwaangamiza wapinzani wetu,” alisema Mirambo.
Mpambano huo utakaoanza saa nane mchana hadi usiku, umeandaliwa na Kampuni za Bob Entertainment na Keen Arts na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi.
No comments:
Post a Comment