15 December 2011

Zungu: Waibueni akina Messi

Na Amina Athumani

WASHIRIKI wa semina ya grassroots, iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA),
wametakiwa kuibua vipaji kama vya akina Leonel Messi wa Barcelona.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu, alisema Messi amepatikana katika timu C ya Bacelona na leo hii kama klabu hiyo itaamua kumuuza itajipatia fedha nyingi.

Alisema endapo kutakuwa na mpangilio wa kufufua vipaji kupitia grassroots, Tanzania itakuwa na wachezaji ambao itawatumia kwa timu ya taifa na baadaye kuwatafutia timu za kulipwa nje ya nchi.

"Mfano mzuri ni mchezaji Kapombe (Shomari) wa Simba, yule hawajamnunua kutoka sehemu yoyote bali ni mchezaji wao wa timu B, hivyo endapo tutakuwa na uvumbuzi wa vipaji kama hivi, hatutakuwa na shida ya kununua wachezaji kwa ajili ya klabu zetu," alisema Zungu.

Alisema mpango huo, ulioanzishwa na TFF pamoja na FIFA wa kufufua vijana wadogo kuanzia umri wa miaka 6, utakuwa ni lulu ya mafanikio katika soka la Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa wachezaji wengi nyota Duniani, wanatokea kwenye groosroots.

Naye Rais wa TFF, Leodegar Tenga amewawasisitiza washiriki hao ambao wanatoka shule za msingi za Mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanavumbua vipaji kupitia mafunzo watakayopewa.

Alisema TFF inatambua kazi ngumu watakayokuwa nayo walimu hao, kutokana na umri wa vijana watakaokuwa wakiwafundisha na kuwataka wazazi, kushirikiana na walimu kuwasapoti watoto ili waweza kujifunza michezo.

Kozi hiyo ya siku tatu itazindua mpango huo rasmi Jumamosi, ambapo kutandaaliwa tamasha la michezo litakalohusisha vijana 1,000 kutoka shule za msingi.

Tenga alisema mpango huo pia utafanyika mikoa yote ya Tanzania na kuwataka wadau wa michezo kudhamini mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment