Na Zahoro Mlanzi
*Yaitimua Malawi
*Kuivaa Uganda nusu fainali
*Viingilio vyazidi kuwa juu
MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Chalenji, timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars),
imefufua matumaini mapya kwa mashabiki wa soka nchini baada ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuichapa Malawi bao 1-0.
Mchezo huo uliokuwa wa kusisimua muda wote wa dakika 90 ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukitanguliwa na mechi nyingine ya robo fainali kati ya Uganda 'The Cranes' iliyoifunga Zimbabwe bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Kili Stars itaumana na Uganda kesho katika nusu fainali ya pili itakayopigwa kuanzia saa 10 za jioni ikitanguliwa na mechi kati ya Rwanda 'Amavubi' na Sudan itakayoanza saa nane za mchana.
Katika mchezo uliowakutanisha Kili Stars na Malawi, timu zote zilianza kwa kila moja kumsoma mwenzake ambapo muda mwingi wa dakika 15 za kwanza mpira ulichezwa sana eneo la katikati.
Kili Stars ilifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 21 baada ya beki Shomari Kapombe kupanda mbele na kupiga krosi safi lakini Ramadhan Chombo 'Redondo' alichelewa kupiga kichwa na kipa Charles Swimi wa Malawi kuokoa.
Malawi ambayo ilicheza taratibu tofauti na ilivyozoeleka, ilifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 24 kupitia kwa Pilirani Makupa ambaye alipokea mpira mrefu uliopigwa na John Banda lakini kabla hajapiga akiwa ndani ya eneo la hatari, Kapombe aliondosha hatari na kuwa kona tasa.
Baada ya shambulizi hilo, Kili Stars ilianza kutakata kwa wachezaji wake kucheza kwa kujiamini na kupiga pasi zenye uhakika ambapo dakika ya 30, Mrisho Ngassa ambaye alikuwa mwiba kwa Malawi alifanya kazi kubwa ya kumhadaa Ndaziona Chatsalira na kupiga krosi iliyotua mguuni mwa Redondo, lakini alipiga shuti dhaifu lililomgonga beki na kutoka nje.
Kili Stars ilizidisha presha langoni mwa Malawi na dakika ya 36, Nurdin Bakari aliwainua vitini mamia ya mashabiki waliojitokeza kwa kufunga bao kwa shuti nje ya eneo la hatari kutokana na pasi safi ya Ngassa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Kili Stars ikiendelea kulishambulia lango la Malawi na dakika ya 51, Ngassa aliwakimbiza mabeki kutoka katikati ya uwanja mpaka ndani ya eneo la hatari lakini wakati akijiandaa kufunga,ghafla beki James Sangala aliokoa.
Malawi nayo ilijibu shambulizi hilo dakika nne baadaye kupitia kwa Banda ambaye alipiga kichwa kilichotoka sentimeta chache golini akiunganisha krosi ya Makupa.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Kili Stars ikionekana kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kutokana na kumiliki mpira muda mwingi lakini safu ya ushambuliaji haikuwa makini kukwamisha mpira wavuni.
Katika robo fainali ya kwanza, bao pekee la Uganda lilifungwa na mshambuliaji, Hamis Kiiza kwa kichwa akinganisha mpira uliopigwa na Sula Matovu na kuiwezesha timu hiyo kutinga nusu fainali.
Katika hatua nyingine, viingilio vya mechi za mashindano hayo vimezidi kupanda ambapo sasa kuziona mechi za nusu fainali kwa kiingilio cha juu ni sh. 20,000 na cha chini ni sh. 3,000.
Kwa mujibu wa taarifa ilizozifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni ni kwamba viti vya bluu na kijani ni sh. 3,000, viti vya machungwa sh. 5,000, viti maalum (VIP B na C) ni sh. 10,000 na VIP A ni sh. 20,000.
Awali kiingilio cha chini kilikuwa ni sh. 1,000 kikapandisha mpaka sh. 2,000 na sasa ni sh. 3,000 huku cha juu wakati michuano inaanza kilikuwa ni sh. 10,000 lakini sasa ni sh. 20,000.
No comments:
Post a Comment