07 December 2011

Mambo ya Ndani nayo yapiga ‘stop’ Kanisa la Nabii Flora

Na Edmund Mihale

MSAJILI wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amevitaka vyombo vya dola kutekeleza agizo la ofisi hiyo kusitisha shughuli za Kanisa la Huduma za Maombezi zinazotolewa  na Nabii Flora Peter Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo linatokana na ofisi hiyo ya msajili kubaini kuwa kanisa hilo limekuwa likiendesha shughuli zake kinyume cha sheria ya vyama namba 337 ya mwaka 2002.

Akizungumza katika mahojiano maalum Majira wiki hii, Mkurugenzi wa Sheria na Malalamiko ambaye pia anashughulikia usajili wa vyama, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Augustine Shio, alisema ofisi yake haijapokea maombi yeyote wala kutoa kibali kwa kanisa hilo kuendesha shughuli zake.


Alisema kuwa kanisa hilo pia limekuwa likiendesha shughuli zake kinyume cha sheria kwani lipo katika eneo ambalo ni la makazi ya watu.

Kwa mujibu wa Bw. Shio, ofisi yake imepokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo wakilalamikia usumbufu unaotokana na shughuli za kanisa hilo kwenye makazi yao.

Hata hivyo, msajili huyo alisema kuwa amesikitishwa na hatua ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kiniondoni Kitengo cha Ardhi kukiuka maagizo ya yaliyotoka Wizara ya Ardhi kwa kuruhusu shughuli za kanisa hilo kundelea ndani ya makazi ya watu.

“Nimeshangazwa na kitendo cha Mkurugenzi wa Manispaa kukaidi mamlaka ya juu yake, maagizo yakishatoka wizarani haiwezekani wilaya kuyatengua,” alisema.

Kwa mujibu wa barua ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kiniondoni ya Oktoba 31 mwaka huu, kanisa hilo lilipewa ruhusa ya kuendelea na huduma zake kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 31 mwaka huu kinyume na barua ya Wizara ya Ardhi ya Oktoba 21 mwaka huu iliyomtaka kiongozi wa kanisa hilo, Nabii Flora Peter kusitisha huduma hiyo mara moja.

Katika barua yake ya Novemba 18 mwaka huu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji, Bi Albina Burra, amesema kuwa kibali hicho cha manispaa ni batili kwa kuwa kimekiuka sheria ya Ardhi namba 8 ya mwaka 2007, kifungu cha 6(3)

Alisema kuwa kifungu hicho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mipango Miji kubadilisha matumizi ya ardhi.

Kutokana na hali hiyo, Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani alisema haitambui huduma hiyo kwa vile haipo katika vitabu vyake vya usajili.


Alisema katika barua yake ametoa nakala kwa uongozi wa Jeshi la Polisi na amewataka wakazi wa eneo hilo kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni  ikiwa kanisa hilo litaendelea kukaidi maagizo ya ofisi ya msajili.

Aidha katika barua yake Msajili amevitaka vyombo vya dola, ikiwemo Idara ya Uhamiaji kuhakiki uraia wa viongozi wa kanisa hilo.

Hata hivyo, alipohojiwa kuhusu suala hilo, Nabii Flora alisema kuwa kanisa lake litaendelea na huduma zake kwani huduma hizo zinahitajika na watu wengi na imesaidia kubadili tabia za vijana wengi ambao walikuwa wakijihusisha na masuala ya uhalifu.

“Haya nayaona kama ni majungu tu ya watu wachache, lakini tutaendelea kutoa huduma na katika jina la Yesu tutashinda,” alisema.

12 comments:

  1. Muhimu ni kufata taratibu za kisheria hujakatazwa ila unaendesha bila kibali halali, na pia unaonyesha kuwa umelaghai baada ya kupewa barua october 21 toka wizarani kusitisha mara moja,ukaenda manispaa kuomba kibali october 31 hapo pia unaonyesha ni ubabaishaji na pia huduma zako ni mfano wa Kikombe cha babu mafuta unayowapa watu muda si mrefu mtaumbuka ama kweli wajinga ndio waliwao!!fata sheria upate kibali halali hata kama ni kwa jina la yesu (Yesu hataki ulaghai)

    ReplyDelete
  2. Neno la Mungu linasema wakati utafika manabii wengi watajitokeza, " Mwenye kusoma na afahamu" sasa kila mmoja atakuwa aliyesoma neno atakuwa anajua ni nini cha kufuata. Someni biblia vizuri ndio jibu la mambo yote.

    ReplyDelete
  3. Huyu "nabii" naye katokea wapi? Kazi kweli kweli!

    ReplyDelete
  4. WATANZANIA TUNAHITAJI KUWA MAKINI NA HAYA YANAYOYOKEA TUKAISHIA KUPATA HASARA. MARA UTASIKIA KWA BABU LOLIONDO WATU KIBAO,MARA DECI WATU KIBAO NA MAKANISA NDO USISEME.HATUNA BUDI KUPIMA KABLA HATUJATUMBIKIA HUMO NA KUPATA HASARA KUBWA. NAWE NABII BASI JITAHIDI KUFUATA TARATIBU ZINASEMAJE KABLA HUJAENDELEA NA HIYO HUDUMA.NENO LA MUNGU LINASEMA WATIINI WENYE MAMLAKA.

    ReplyDelete
  5. NINAAMINI SERIKALI INAPENDA WATU WANAOSAIDIA KUELIMISHA JAMII NA KUPUNGUZA UHALIFU KAMA NA BII HUYO ANAVYOSEMA AMEWAELIMISHA VIJANA KADHAA KUTOKA KWENYE UHALIFU HILO NI JEMA KABISA, BUT NI VIZURI ZAIDI KAMA NABII HUYO ATATAFUTA MWANA SHERIA ATAKAYE MUELIMISHA JINSI YA KUPATA KIBALI TOKA WIZARANI CHA KUENDESHA HUDUMA YAKE NA KUEPUKA MIGOGORO ISIYO YA LAZIMA, SERIKALI YETU HAIZUII UHURU WA KUABUDU NA KUAMINI KAMA ATAKAVYO MTU, NDIO SABABU KATIBA IMEWEKA UHURU HUO SUALA ZIMA NI KUFUATA TARATIBU TU!
    INAWEZEKANA HUYO MKURUGENZI ALITOA KIBALI CHA MUDA ILI NABII HUYO AKAMILISHE TARATIBU ZA USAJILI. ASIPO KAMILISHA TARATIBU HIZO SASA ITAKUWA NI TATIZO JINGINE NA LITA MGHARIMU NABII HUYO NA WAFUASI WAKE.
    NCHI YETU TUNATABIA YA KUVUMILIANA UTAKUTA KANISA AU MSIKITI UMEJENGWA KARIBU NA DIRISHA LAKO NA WATAANZA IBADA KWA MUDA AMBAO UMEPUMZIKA ITABIDI UVUMILIE SAUTI ZA SPIKA HATA KAMA NDIO UNATAKA KULALA, KWA SABABU IMANI HIYO NA MSIKITI HUO UPO KISHERIA NA WAMEFUATA TAATIBU ZOTE, NA PIA IMANI HIZO ZOTE NI MSAADA KWA UMA NA KWA SERIKALI YETU, IKIWA ZITAFUATA SHERIA ZILIZOPO.
    AIDHA NI VYEMA KUFAHAMU KUWA NCHI NYINGINE HAKUNA UHURU WAKUABUDU NA KUAMINI HADHARANI KAMA ILIVYO HAPA TANZANIA MFANO BAADHI YA NCHI ZA MASHARIKI NK. HUKO IMANI NI MOJA TU ILIYOPITISHWA NA SHERIA INAFUATWA.
    NASI TUFUATE SHERIA ZETU HATA KAMA ZINA MAPUNGUFU AU HAZIPENDEZI BAADHI YA WATU NI KUVUMILIANA NA KUTII SHERIA.

    NI MIMI MTU WA WATU WA TUELIMISHANE.

    ReplyDelete
  6. Mimi naona hivi vita anavyopigwa huyu "Nabii" ni kwa maslahi ya watu fulani kwenye mamlaka husika. Huduma yake inasaidia sana jamii, hasa vijana ili wajirudi na kubadili mienendo yao na kuwa raia wema katika jamii. Eneo la Mbezi beach kuna majumba ya starehe yaliyojengwa katikati ya makazi ya watu. Siyo 'sound proof' na kila kunapokua na sherehe-harusi, send-off, kitchen party, n.k. watu hawasikilizani kutokana na muziki na kelele nyingine. Inajulikana wazi kwamba wenyewe wanakingiwa kifua na wakubwa na hata vibali vyao si halali. Naongelea maeneo kama Valentino Hall, karibu na NSSF

    ReplyDelete
  7. Neno la Mungu ni lazima lieleweke kwa kila binadamu hasa wale walio karibu sana na kanisa ili wao walisambaze mbele lakini taratibu ni lazima zifuatwe ili tuweze kuishi in harmony.Huwezi kutangaza neno uko juu ya paa la nyumba ya mtu, labda akuruhusu yeye.Huu ni mfano wa taratibu. Namsihi apate mwanasheria wa kumshauri.

    ReplyDelete
  8. HAO NI MANABII WA UWONGO WANATUMIA BIBLIA KWA MANUFAA YAO NA KUWADANGANYA WANANCHI KUJIPATIA PESA NYINGI ISIVYO KIHALALI. HUYO NABII ANAFAA KUFUNGIWA NAKUCHUNGUZWA ZAIDI KWANI WAKO WENGI HAO

    ReplyDelete
  9. Tatizo sio nabii bali ni haki itendeke

    ReplyDelete
  10. Mimi sielewi kwa nini nchi isiyo na Dini inazuia huduma za watu. Najua Watanzania wengi ni wagonjwa na wanadanganyika sana wanaposikia kuna mahali watapata faraja. Pia wengi ni maskini na wanaishi maisha ya taabu, hivi dini inakuwa ndiyo kitulizo chao. La msingi siyo kumkataza bali ni kumpa taratibu zinazohitajika na aendelee na shughuli hii ya kinabii. Mbona kila mahali kumejaa misikiti na inawapigia watu kelele kila siku saa 10 usiku na hakuna anayesema chochote? Usumbufu ungepewa tafsiri sahihi. Kama kwa Flora basi na wengine wote hasa wanaoendesha shughuli zao usiku. Ukienda Ulaya utaona utlivu wa watu nitofauti na sisi, kwani hawana shida za kimaisha. wanaotaka kusali huru na wasiosali huru. Someni aliyosema Gamaliel katika kitabu cha Matendo ya Mitume. "Ikiwa ni kwa nguvu ya Mungu hatuweza kushindana naye, lakini ikiwa ni kwa nguvu ya mwanadamu kazi hiyo itaisha tu, mwacheni na wala msimlazimishe kuacha" ni shida za watu zinawapeleka kwa Mungu. Mambo yakiwa sawa na uchumi ukipanda kidogo shughuli hizo zitaisha tu. Kazi kwenu viongozi wa serikali. Ni wazi kuwa kama sipendi au nikisukumwa na wivu lazima niseme tu ubaya ili mwenzangu asifanikiwe. Chonde chonde mwacheni aendelee na kazi ya Mungu.

    ReplyDelete
  11. Msemaji hapo juu jitahidi basi kuelewa,hakuna aliyemzuia kufanya kazi njema ya Mungu ila hajafuata taratibu, tukisema kila mmoja afanye anavyotaka mladi tu ni kazi ya Mungu unafikiri maisha yataenda?

    ReplyDelete
  12. Maandiko matakatifu yanasema heshimuni mamlaka zilizowekwa.Ni muhimu kwa huyo 'NABII' kupata baraka za mamlaka husika kwa kuzingatia utaratibu unaopaswa kufuatwa

    ReplyDelete