07 December 2011

Wafanyabiashara waomba VAT kupunguzwa

Na Grace Ndossa

WAFANYABIASHARA wa sekta binafsi wameomba serikali kupunguza ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi 15

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na mwakilishi wa wafanyabiashara wa sekta binafsi, Bw. Ndibalema Mwanjani katika maadhimisho ya tano ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya siku ya mlipa kodi.

Alisema kuwa kama serikali itapunguza kodi hadi kufikia asilimia hizo watajiendesha  bila kutetereka na kulipa kodi kwa wakati.

Pia wameitaka serikali, idara zake na taasisi binafsi wasinunue samani kutoka nje kwani kuna viwanda hapa nchini vinavyotengeneza bidhaa hizo na zenye ubora kama za nje.

"Kama serikali itanunua bidhaa za hapa nchini itaongezea pato la nchi yetu, ajira kwa vijana na ulipaji kodi utaongezeka," alisema Bw. Mwanjani.

Pia alisema kuwa kwa pamoja wafanyabiashara wameamua hawatatoa tena rushwa watafanya kazi na watu wa kuzuia na kupambana na rushwa.

"Maamuzi hayo yanahitaji ujasiri mkubwa  kwani wengi watakosa kazi kutokana na uadilifu wake," alisema.

Naye Waziri wa Fedha akisoma risala kwa niaba ya Rais Kikwete alisema kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania wamekusanya kodi kutoka sh. bilioni 42 mwaka 1996 hadi sh. bilioni 500.

Alisema kuwa kiasi hicho ni kikubwa kwani wamepiga hatua na kwa mwaka huu wamekusanya jumla ya sh. bilioni 604.

No comments:

Post a Comment