Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), inatarajia kufungua pazia la mashindano ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup), kwa kuumana na
Zanzibar (Zanzibar Heroes), katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Aman, visiwani humo.
Timu hizo zitaumana kwa mwaliko maalumu kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), katika kupamba sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya mapinduzi visiwani humo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimepatikana jijini Dar es Salaam jana, zilieleza kwamba timu hizo zimepewa heshima hiyo ili kuyafanya mashindano hayo yazidi kupewa heshima kutokana na tukio lenyewe.
“ZFA imeiandikia barua TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), kuiomba timu yao ya taifa ya Bara, icheze na ya visiwani katika kufungua mashindano ya Kombe la Mapinduzi, hivyo tunasubili majibu kutoka kwao na tuna imani hilo litafanikiwa,” alisema mtoa habari huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alikiri kupokea barua ya mwaliko kutoka ZFA lakini bado suala hilo linashughulikiwa na kamati husika.
“Ni kweli tumepokea barua ya mwaliko kutoka ZFA ikihitaji mechi hiyo (Kili Stars na Zanzibar Heroes zifungue Mapinduzi Cup), lakini bado haijaamuliwa kwani Kamati ya Mashindano ndio inalishughulikia na keshokutwa (Jumatano), ndio tutaweka wazi,” alisema Wambura.
Mashindano ya mwaka huu yamepangwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, mwakani ambapo kilele chake ambapo itapigwa fainali ni Januari 12 ambayo ni siku ya mapinduzi visiwani humo kila mwaka.
Bingwa mtetezi wa mashindano hayo ni Simba ambayo katika fainali ya mapema mwaka huu iliwachapa wapinzani wao wa jadi, Yanga kwa mabao 2-0 ambapo fainali hiyo ilipigwa Uwanja wa Amaan, visiwani humo.
Simba, Yanga na Azam FC ndizo timu zilizoteuliwa kushiriki mashindano hayo kwa mwaka huu lakini mpaka sasa ni Azam pekee ndio iliyotoa jibu la moja kwa moja kushiriki mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment