15 December 2011

BMT kuinyoosha CHAMIJATA

Na Amina Athumani

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), litaanza kutoa makucha yake kwa viongozi wa Chama cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA), ambao kutokana na kukaa madarakani muda mrefu na kushindwa
kufanya uchaguzi.

Akizungumza kwa simu Dar es Salaam jana Msemaji wa BMT, Maulid Kitenge alisema hawatavifumbia macho vyama vyote, vinavyoendeshwa kienyeji.

Alisema vyama vyote vilivyopo chini ya BMT ni lazima vifuate kanuni na sheria za katiba hiyo na si viongozi kujimilikisha vyama.

Kitenge alisema BMT itashughulikia vyama vyote visivyofuata kanuni za baraza hilo na wanachosubiri ni ratiba ili kuanza utekelezaji wa kuvihoji vyama.

CHAMIJATA ambayo ipo chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed Kazingume ambaye ni mwasisi wa chama hicho, amekiongoza tangu mwaka 1975 bila kufanya uchaguzi wa viongozi wapya.

Kwa mujibu wa Kazingumbe, anasema si kwamba hawataki kufanya Uchaguzi Mkuu, bali ni kutokana na kukabiliwa na ukata wa fedha.

"Mfano mzuri sisi CHAMIJATA, tumeandaa uchaguzi ambao tulipanga ufanyike Oktoba 15 mwaka huu (leo), lakini hatuna fedha na mimi ndiye mwasisi wa chama hiki nitamwachia nani bila kufanya uchaguzi?" alihoji Kazingumbe.

Alisema kikwazo kikubwa kinachokwamisha yeye kuendelea kuongoza hadi leo ni kutokana na kukosa fedha za uchaguzi.

No comments:

Post a Comment