Na Mwali Ibrahim
SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), linatarajia kutoa programu yake kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya kufuzu mashindano ya Olimpiki
yatakayofanyika mwakani London, Uingereza.
Mashindano hayo ya kufuzu kwa nchi za Afrika yanatarajia kufanyika Aprili 27, mwakani nchini Mexico.
Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga, alisema wameamua kuiweka wazi programu hiyo ili iweze kuchangiwa na wadau wa ngumi, ili kufanikisha timu ya taifa kushiriki katika mashindano hayo.
Alisema ratiba ya michuano hiyo wataiweka wazi wiki ijayo, ili kila mtu aweze kuiona na kutoa mawazo yao na kuichangia kwa manufaa ya mchezo wa ngumi na taifa kwa ujumla.
"Tumeamua kufanya hivyo ili iwe rahisi kwa wadau wote kujua nini kinaendelea na pia tunahitaji mchango wao kwani BFT, peke yetu hatutaweza kumudu kila kitu kuchangia kwao kutasaidia timu kushiriki katika mshindano hayo," alisema Makore.
Alisema hiyo itasaidia pia kuepusha lawama kwa BFT, siku ya mwisho timu ikishindwa kushiriki lawama ziwe kwa nchi nzima na si kwa BFT.
Alisema kwa sasa mabondi wote, wanaendelea kujifua kila mtu kivyake, kabla ya kukaa kambi ya pamoja kwa ajili ya mashindano.
No comments:
Post a Comment