TOYOTA, Japan
TIMU ya Al Sadd ya Qatar,imetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa klabu, baada ya kuilaza, Esperance ya Tunisia na hivyo kujipeleka kinywani
mwa mabingwa wa Hispania, Barcelona.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jana, Esperance ilikitawala kipindi cha kwanza,lakini ilikuwa ni Al Sadd iliyofanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 33, kutokana na mpira wa krosi iliyochongwa na mchezaji, Kader Keita kutoka upande wa kulia mwa uwanja huku mlinda mlango wa Esperance, Moez Ben Cherifia akiifuata bila mafanikio na mpira kutua kichwani mwa Khalfan Al Khalfan.
“Esperance walikuwa ni wazuri dakika 10 za kwanza za mechi,”alisema kocha wa Al Sadd, Jorge Fossati. “Waliweeza kudhibiti mpira na kupigiana pasi nyingi hususani katika sehemu ya kiungo,hivyo nikaamua kubadili mchezo na tukaweza kudhibiti vyema mpira na kuweza kufanya mashambulizi ya kushutukiza,”aliongeza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani AP, Al Sadd walioongeza bao la pili dakika nne baada ya timu hizo kutoka mapumziko kufuatia shuti la kushutukiza la mchezaji Abdulla Koni, aliyeunganisha pasi ya mchezaji Al Khalfan.
Baada ya kupachikwa mabao hayo, Esperance ilikuja juu kutaka kusawazisha na jitihada hizo zilifanikiwa kuzaa matunda baada ya nahodha wa timu hiyo Ousama Darragi kujitwisha mpira wa adhabu iliyochongwa na Khelil Chammam.
Mabingwa hao wa Tunisi waliingia katika mchezo huo kwa kuwakamia wapinzani wao na kuna mabao mawili ambayo waliyapata lakini yakakataliwa na mwamuzi baada ya wafungaji kuwa wameotea.
Dakika ya 79,mchezaji Yannick Ndjeng alionekana kama angesawazisha lakini alikuwa ameotea huku mchezaji Khaled Ayari naye akimchambua mlinda mlango wa Al Sadd, Mohamed Saqr dakiza za nyongeza lakini ikaamliwa na mwamuzi kutoka Chile, Enrique Osses kwamba alikuwa ameotea.
No comments:
Post a Comment