12 December 2011

Micho: Chalenji ni kipimo kizuri kwa maandalizi

Na Speciroza Joseph

Baada ya kushindwa kutwaa Kombe la Chalenji, Kocha Mkuu wa timu ya Rwanda 'Amavubi', Sredojevic Micho, amesema michuano hiyo kwake ni kama sehemu ya
mandalizi na kujiweka sawa kwa ajili ya michuano mingine ya kimataifa.

Alitoa kauli hiyo juzi maara baada ya kumalizika kwa fainali ya michuano hiyo iliyofanyikia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo timu yake ilichapwa kwa penalti 3-2 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.

“Tumepigana kufa na kupona kutwaa ubingwa, naamini haikuwa bahati yetu wenzetu Uganda walikuwa na bahati, mashindano haya yana umuhimu mkubwa kwa timu yangu, kwa muda wote tumeweza kujenga timu imara na nzuri” alisema Micho.

Micho aliongeza kuwa kupoteza mchezo wa fainali, hautakuwa na nafasi ya kupoteza morali kwa timu zaidi ni kuongeza kujiamini na uwezo kwa wachezaji wake ambao wanajiandaa na michuano mingi ya kimataifa ikiwemo kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, michuano ya CHAN na Kombe la Mafaifa ya Africa.

Akizungumzia michuano kwa ujumla, Micho alisema mashindano yalikuwa ya kiwango cha juu, timu zilikuwa vizuri na kuboreshwa kwa michuano hiyo itakuwa sehemu nzuri ya kukuza na kuendeleza soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Alisema kupewa tuzo ya kocha bora wa mashindano hayo ni heshima kwake na ataitumia kama ngao ya kuweza kufanya vizuri kwa timu hiyo.

Rwanda wametwaa nafasi ya pili ya michuano ya kombe hilo, Uganda wakiwa mabingwa wapya na Sudan wakiwa nafasi ya tatu.

Mbali na kuwa katika nafasi hiyo, Rwanda imekuwa timu pekee katika michuano hiyo kuwa na washindi wa nafasi tofauti wametoa, kocha bora ambaye ni Micho, mchezaji bora Haruna Niyonzima na wafungaji bora wawili Kagere Medie na Olivier Karekezi.

No comments:

Post a Comment