06 December 2011

Ajali mbaya yaua 8, kujeruhi 18 Shinyanga

 Na Suleiman Abeid, Shinyanga

*Nyingine yatokea Mbeya, yaua 3, dereva akimbia.

WATU sita wamekufa papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 12 alfajiri katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Salawe, wilayani Shinyanga likihusisha basi la Kampuni ya Bedui T 430 AFN, aina ya Scania.

Akizungumza na Majira katika Hospitali ya Serikali mkoani hapa, dereva wa basi hilo, Bw. Fabian Josephat (37), alisema chanzo cha ajali hiyo ni kipande cha barabara kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

“Wakati nikiendelea na safari, nilipofika eneo la ajali nikakuta maji yakikatiza barabarani baada ya hapo nilisikia kishindo kizito baada ya gari kuingia katika shimo,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, alishindwa kufunga breki hivyo kusababisha gari kupinduka.

“Kwa kweli sielewi lolote jinsi ajali ilivyotokea maana nilipofika eneo la Manghu (Kijiji cha Songambele), niliona kuna maji yanakatisha barabarani, nilihisi ni maji ya kawaida kutokana na hali ya giza kwa sababu kulikuwa hakujapambazuka vizuri.

“Glafla nilisikia gari limekita ndani ya shimo, niliona gari imepaa na kupoteza mwelekeo hivyo sikuweza kulimudu likapinduka upande wa pili wa barabara,” alisema Bw. Josephat.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Diwani Athumani, aliwataja watu waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Bw. Juma Lukanda (30), mkazi wa Msalala, Bw. Hussein Lukwa (57), mkazi wa Lyabusalu na George Machibya (55), mkazi wa Shinyanga mjini.

Wengine ni Bw. Anzenti Masanja (20), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Gembe, Bw. Clement Kashindye, Mganga katika Hospitali ya Ilola na mkazi wa Salawe, wilayani Shinyanga mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Bi. Hayo, mwenye umri kati ya miaka 15-25, mkazi wa Kijiji cha Mwabenda.

Kamanda Athumani alisema, chanzo cha ajali hiyo ni dereva kutokuwa makini wakati huu wa mvua nyingi zinazonyesha mkoani humo hali ambayo ilisababisha ashindwe kumudu gari baada ya kukuta sehemu ya barabara imekatwa na maji.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Serikali mkoani hapa, Dkt. Fredrick Mlekwa, alikiri kupokea majeruhi 18 na kusema sita kati yao, walikuwa na hali mbaya baada ya kuvunjika sehemu mbalimbali za miili yao.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni pamoja na dereva wa basi hilo Bw. Josephat, Ofisa Muuguzi Hospitali ya Mkoa huo, Bi. Celina Mpemba (36) na mwanaye mdogo Joachim Mkina (7).

Wengine ni Bw. Shija Kishamapanda (40), Bw. William Joseph (35), Bw. Johnson Gabriel (41), Bi. Winfrida Leonard (25), Bi. Leokadia Mathias (37), Bi. Mary Marco Simbila (50), Bw. Marco Sabulile (50), na Bi. Maria Joseph (21).

Abiria wengine waliojeruhiwa ni Bw. Felix Donald (23), mkazi wa Ngokolo Shinyanga, Bw. Mikidadi Juma (19), mkazi wa Bugayambelele, Bw. Hassan Shabani (11), mkazi wa Manghu Salawe, Bw. Reuben Buzuka (61), mkazi wa Salawe na Bi. Kulwa Thomas (48), mkazi wa Ipango.

Wengine ni Bi. Tatu Ally (50) na Bi. Rehema Said (30), wote wakazi wa Kijiji cha Manghu Salawe na Bi. Mbula Masalamunda (45), mkazi wa Kijiji cha Lubale.

Wakati huo huo, Rashid Mkwinda kutoka Mbeya anaripoti kuwa,
watu watatu wamekufa papo hapo na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya basi dogo la abiria Hiace maarufu 'Kipanya', T 173 AWF, lililokuwa likitokea Mbeya mjini kwenda Tunduma.

Basi hilo limegongana na lori aina ya Scania T 357 BBV, ambalo lilikuwa likitokea nchi jirani ya Zambia.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:45 jioni katika eneo la Mahenje, ambapo dereva wa Hiace, alipoteza mwelekeo na kuliingia lori ambalo liligonga kipanya hicho ubavu wa kulia.

Wakizungumza na Majira, baadhi ya abiria wa basi hilo ambao walijeruhiwa katika ajali hiyo, walisema wakati basi hilo likipandisha mlima wa Senjele, dereva wao aliyefahamika kwa jina la Stanley Sengo, alipigwa na jua usoni na baada ya kufika eneo la tambarare ghafla akapoteza mwelekeo na kujiingiza upande wa lori.

Mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya mjini Vwawa, wilayani Mbozi, Dkt. Frank Mwakyolo, alisema amepokea miili ya watu watatu ambao hadi juzi usiku, walikuwa bado hawajafahamika majina yao pamoja na majeruhi sita.

Alisema mmoja wa majeruhi ni dereva wa basi hilo Bw. Sengo (33), ambaye alijeruhiwa mkono wa kulia na mbavu lakini alitoroka wodini usiku wakati akiendelea na matibabu.

Aliongeza kuwa, miili ya  abiria hao ilitambuliwa jana mchana na ndugu zao ambapo mmoja wa marehemu ni mke wa Mchungaji wa Kanisa la Moravian, Jimbo la Kusini aliyefahamika kwa jina la Bi. Rehema Mwanda (42).

Kwa mujibu wa shemeji wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mrotwa Msyaliha, alisema marehemu ni mke wa kaka yake ambaye ni Mchungaji wa kanisa hilo, Sevirwe Msyaliha, mkazi wa Kijiji cha Mbozi Misheni.

Wengine waliokufa ambao wametambuliwa na ndugu zao ni pamoja na Bw. Efrahimu Mlawizi (31), mkazi wa Ilolo na Bw. Chepela Mumwa, mkazi wa Iwalanje.

No comments:

Post a Comment