06 December 2011

Chenji ya rada yatua serikalini.

 Na Mwandishi Wetu
*Ni bil.80, Mkulo azitolea ufafanuzi

 HATIMAYE Serikali ya Uingereza imetimiza ahadi ya kuirudishia Tanzania Paundi milioni 29.5 sawa na sh.bilioni 80 za kitanzania
kama malipo ya ziada yaliyotolewa kinyume cha utaratibu kwa kampuni inayouza vifaa vya kijeshi ya BAE Systems katika manunuzi ya rada.

Tayari Serikali imeelekeza fedha hizo zipelekwe katika sekta ya elimu ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa kama ukosefu wa nyumba za walimu, maabara na vifaa vyake, madarasa, vitabu na walimu wa kutosha.

Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mkulo, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari ofisini kwake waliotaka kujua hatua iliyofikiwa na Serikali katika kudai fedha hizo.

Bw.Mkulo alitoa ufafanuzi huo baada ya kupokea msaada wa sh. bilioni 3.2 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa Tanzania kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Serikali za Mitaa nchini.

“Ninachopenda kusema ni kwamba, tayari fedha za rada zimetolewa na Serikali ya Uingereza ila tunasubiri kukaa kikao ili tujue katika sekta hiyo ya elimu zinatumika vipi.

“Tumeichagua sekta hii kwa sababu inakabiliwa na changamoto nyingi na wananchi wamekuwa wakiilalamikia sana sasa ili wajue kuwa fedha hizi zimelipwa ni vyema tukaziweka katika elimu ili iweze kunufaisha wananchi,” alisema Bw.Mkulo.

Aliongeza kuwa, kikao cha kuamua maeneo ambayo fedha hizo zitaelekezwa katika sekta hiyo, kitahusisha Wizara ya Fedha, Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ubalozi wa Uingereza na Wizara ya Elimu yenyewe.

“Lengo lingine la kupeleka fedha hizi katika elimu ni kutaka wananchi watambue kuwa, tayari tumelipwa fedha hizi na zitatumika katika shughuli za maendeleo ya nchi.

“Matumizi ya fedha hizi yatamaliza taarifa za uzushi za kuwepo kwa vitendo vya rushwa,” alisema.

Sakata la malipo ya fedha za rada zilizolipwa kwa kampuni hiyo, zimekuwa gumzo kwa makundi mbalimbali ya watu nchini baada ya kugundulika kuwa, kampuni hiyo iliitoza Tanzania bei kubwa zaidi ya ile iliyotakiwa.

Bunge la Uingereza limekuwa mstari wa mbele kuitetea Tanzania ili iweze kurudishiwa fedha hizo na kupendekeza Serikali ya nchi hiyo kuitoza faini kwa kitendo cha kuinyonya nchi maskini kama Tanzania na kuagiza kurejeshwa kwa fedha hizo.

Hivi karibuni, Bunge hilo lilipendekeza wahusika wote waliofanikisha Tanzania kulipa fedha nyingi kuliko bei halisi ya rada, wachukuliwe hatua bila kuachwa.

Kampuni ya BAE iliiuzia Tanzania rada hiyo kwa dola za Marekani milioni 40 (sh. bilioni 54), hatua iliyopingwa na wengi, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Uingereza wa Masuala ya Afrika, Bw.Clear Shot,  pamoja na taasisi mbalimbali ikiwamo Benki ya Dunia (WB).

5 comments:

  1. Wahaini wa uzalendo waliotaka pesa hizi zisirudishwe mmeangukia pua. Nyie ni wajinga tu mnaosaliti nchi. Nchi inasalitiwa,inamalizwa na wahujumu uchumi na nyie mnatia petroli kwenye moto ili iangamie kabisa.Kidole kikiuma hakikatwi kinatafutiwa tiba.

    ReplyDelete
  2. Ni lazima wale wote waliohusika na ufisadi huo wachuliwe hatua haraka. Serikali ili kurudisha imani kwa wananchi, ni lazima ifanye kazi yake. Kinachofanya wananchi wengi wanalalamika ni kutothubutu kwa dhati, sio kwa maneno tu. Lazima watu wathibitishe kweli huku ndo kuthubutu na sio mifano rahisi tu. Kujenga imani kwa wananchi kunataka firmness kwenye kuchukua hatua za kweli na sio maneno.

    ReplyDelete
  3. Kuna mtazamo kuwa viongozi wa serikali wanalalamikiwa na wananchi kuwa kuna tabia ya kulindana kwenye kashfa kubwa kama hizi. Tafiti nyingi zilizofanywa na watu makini, zinaonyesha kuwa madhara yake ni makubwa sana huko mbeleni kuliko kuonekana mwema kwa watu wachache ambao huwezi kuzikwa nao pamoja ukifa.Hukuna haja ya kupata cheap popularity kutoka kwa watu wachache. Kinachofanyika kule ICC, ndo kuthubutu.Kujiweka safi kama Mwalimu Nyerere kwa kuwachulia watu hatua za kweli kunahitaji umakini. Siasa za ndani huko mbeleni kabla ya 2015 zitakuwa ngumu mno kama hatua kadhaa hazitachukuliwa sasa hivi.

    ReplyDelete
  4. Tunashukuru kuzipata pesa zetu.Niwaombe ndugu zetu ambao wanahusika na ununuzi wa vifaa au huduma za serikali,wawe waangalifu na waache uroho,mnatuumiza sana Watanzania wenzenu.Na bila shaka kama kuna waliohusika na uhuni huu, lazima sheria ichukue mkondo wake.

    ReplyDelete
  5. MEMBE ALIWAHI KUSEMA KUWA HAKUNA PESA ZILIZOIBIWA KATIKA ISSUE YA RADAR LEO VIPI ANASEMAJE KUHUSU PESA KURUDISHWA NA WEWE MCHANGIAJI WA KWANZA HAKUNA AIYETAKA PESA ZISIRUDISHWE WATU WALIKUWA WAPINGA PESA KURUDISHWA KWENYE MIKOO YA WEZI WALEWALE WALIOIBA MARA YA KWANZA.

    ReplyDelete