17 October 2011

Manji aivutia pumzi Yanga

Na Zahoro Mlanzi

ALIYEKUWA Mfadhili wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji ametua nchini jana alfajiri akitokea Marekani na kutaka apewe wiki moja atafakari
juu ya kusaini mkataba mpya wa kuifadhili tena timu hiyo.

Hali hiyo imetokana na uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti, Llody Nchunga kumwandikia barua mfadhili huyo kumuomba arejee Yanga kuokoa jahazi.

Wakati Nchunga akiwaza hilo, wiki iliyopita wachezaji wa timu hiyo ilidaiwa kugomea mazoezi wakishinikiza walipwe mishahara yao wanayoidai klabu hiyo.

Akilithibitishia gazeti hili Dar es Salaam jana juu ya ujio wa Manji, Ofisa Habari wa klabu hiyo Louis Sendeu, alisema kweli ameshatua nchini lakini kwanza anataka kukutana na wazee wa klabu na Kamati ya Utendaj ndipo mengine yafuate.

"Ni kweli amekuja na hajasaini mkataba, ila ametoa wiki moja kwanza aangalie wapi kwa kuanzia maana kuna mambo mengi anataka kufanya kwa sasa.

"Kuna Uwanja wetu wa Kaunda unatakiwa umaliziwe, tuna kiwanja mtaa wa Mafia ambacho tunataka kujenga kitega uchumi, hivyo ukiangalia kiukweli mambo ni mengi," alisema.

Alisema baada ya kukutana na wazee wa klabu pamoja na viongozi na kujadili kwa kina na kufikia muafaka, ndipo atakaposaini mkataba mpya baada ya awali kujiondoa.

Manji alijiondoa katika kuifadhili timu hiyo kutokana na viongozi wa klabu hiyo, kudaiwa kuzitumia vibaya fedha zilizotolewa kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Kagame.

Mbali na fedha hizo, pia ilidaiwa walizitumia vibaya fedha za usajili na hata baadhi ya wachezaji kushindwa kulipwa baadhi ya marupurupu yao.

3 comments:

  1. Hao viongozi wa Yanga ni wababaishaji wakubwa, Manji alipokuwa anaisaidia timu, wao walitumia usanii na utapeli kujinufaisha na fedha hizo bila kuwafikia wachezaji. Alipoomba ufanyike ukaguzi wa mapato ikawa balaa kubwa hadi kufikia kujiuzulu. Manji asikubali kufadhili timu mpaka aweke misingi mizuri ya uwajibikaji kwa fedha anazotoa, asidanganywe na kupokewa kwa nderemo hiyo ni janja ya kuingizwa mjini !

    ReplyDelete
  2. Kweli inasikitisha sana kuona watu wazima wenye akili timamu macho mawili,mikono miwili,miguu miwili wanashindwa kukaa chini na kubuni jinsi ya kuanzisha miradi itakayo wezesha kuiendesha timu kibiashara na kuiwezesha Yanga kama Yanga kujitegemea yenyewe kama ilivyo Al ahli,Asec mimosa,Espirence na tumu nyingine nyingi tu barani Afrika.Hebu tuangalia hapa jirani na sisi wala tuende mbali sana,Angalia leo hii TP Mazembe wanandege mbili kwa ajili ya kusafirishia wachezaji,Wana hospitali ya kisasa kwa ajili ya wachezaji na sehemu nzuri sana kwa ajili ya malazi kwa wachezaji.Yote haya hayatokani na kutegemea mapato ya malangoni kama ilivyo kuwa kwa timu zetu za Tanzania.Tuchukulie mfano mzuri kutoka Yanga.Wana jengo kubwa la kutosha kuvifanyia vyumba vyake matengenezo mazuri kwa ajili ya malazi kwa wachezaji pamoja na uwanja wao wenyewe kwa ajili ya mazoezi na hata kuwaka kambi kwa ajili ya mashindano mbalimbali.Lakini badala ya kuboresha jengo pamoja na uwanja wanakwenda kupiga kambi sehemu nyingine kabisa ambapo inabidi walipie malazi kwa ajili ya timu alafu mwisho wa siku wanashindwa hata kulipa gharama na inabidi saa nyingine timu izuiliwe kutoa ilipo kwenda kucheza mchezo unaowasubiri na kuamua kuweka basi rehani ili timu iruhusiwa kwenda uwanjani.Hii ni aibu gani hasa kwa timu amboyo imeanzishwa mwaka 1935 lakini mpaka leo hii haiwezi kujitegema yenyewe.Sasa nauliza swali hivi Manji akifa basi ndio mwisho wa Yanga?au Wataanza kuhangaika kutafuta mfadhili mwingine?na je watakuwa ombaomba mpaka Lini?

    ReplyDelete
  3. Anonymous wa October 17, 2011 2:37 PM, yaani umeongea ukweli. Mie kama mtu mmoja naye support sana mpira bongo nilisema haya kama miaka 15 iliyopita kwamba hizi timu inabidi ziwe na vitega uchumi, lakini jamaa wa Yanga walibisha kata kata. Leo nasimama pembeni naangalia jinsi wanavyohangaika, na timu nyingine kama Tukuyu Stars zimekufa kabisa. Yanga na Simba wanavitega uchumi mwingi, kwa mfano wakikarabati majengo yao yakawa hostel au hotel, sisi wote tungekaa pale kuwasupport. Yaani jamaa uongozi ni bongo hamna sio wabunifu. Timu hizi kila kitu wanapewa toka kwa wadhamini. Huu mtindo unaua maendeleo, kwani pale mdhamini anapojitoa basi timu nayo imekwisha. Inabidi twende na wakati jamani, kwani hata timu za Uingereza kibao na ubishi wao walikubali matokeo timu zao sasa zimenunuliwa na Wamerikani.

    ReplyDelete