17 October 2011

Magavana EAC wakubaliana kusimamia mfumko wa bei

Na Godfrey Ismaely

MAGAVANA wa Benki Kuu katika nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamekubaliana kusimamia mpango
maalum wa kutaratibu shughuli ya kukabiliana na mfumuko wa bei katika bidhaa za chakula na mafuta kupitia kanda yao.

Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ni pamoja na Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki kwa vyombo vya habari na Idara ya Mahusiano ya Umma na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania (BOT) maamuzi hayo yalifikiwa wiki iliyopita na magavana hao wakati wa mkutano wao  uliofanyika Nairobi nchini Kenya.

"Magavana wa benki kuu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, waliona kwamba kanda yetu inakabiliwa na asili ya mfumuko wa bei ya juu sana hasa kwa upande wa chakula na bei ya mafuta lakini pia kutokana na mahitaji ya shinikizo," ilifafanua taarifa hiyo.

Magavana hao walikubaliana kuratibu mpango ambao utajikita katika maeneo maalum matatu hususani kuimarisha sera ya fedha, kuzuia hali tete katika masoko ya fedha za kigeni ikiwemo kukabiliana na changamoto mbalimbali katika fedha za uvumi.

"Magavana waliohudhuria mkutano huo ni Profesa Benno Ndulu Benki Kuu Tanzania, Profesa Njuguna Ndung'u Benki Kuu ya Kenya, Profesa Tumusiime Mutebile Benki Kuu Uganda, Balozi Claver Bagaragaza Benki ya Taifa ya Rwanda na Bw.Gaspard Sindayigaya Benki Kuu ya Burundi," iliongeza taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine taarifa hiyo ilieleza kuwa katika tamko la pamoja magavana hao wa EAC pia waligundua kwamba kanda ya Afrika Mashariki inakabiliwa na shinikizo la juu kudhoofika kwa thamani ya fedha.

"Shinikizo la sarafu kudhoofika kunatokana na upanuzi wa upungufu wa sasa katika akaunti inayotoka na upanuzi wa haraka wa muswada wa kuagiza mafuta na bidhaa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu," ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment