17 October 2011

UWAKA wachanga mil. 44 kusaidia Masista wadogo

Na Peter Mwenda

WANAUME Wakatoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam (UWAKA) wamechanga sh. milioni 44 kwa ajili ya kusaidia masista wadogo wa
Shirika la Mtakatifu Francisco wa Asizi, Mbagala.

Katika harambee hiyo iliyongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Saltarus Libena, Parokia iliyoongoza kwa michango hiyo ni Segerea iliyotosha sh. milioni 2.6.

Akitoa shukrani kwa msaada huo Mama Mkuu wa Masista wa Shirika la Dada wadogo wa Mtakatifu Francisco wa Asizi, Sista Coletha Paulo, alisema msaada huo utasaidia kufungua miradi ambayo ilisimama kutokana na ukosefu wa fedha.

Alisema miradi ya ufugaji ng'ombe unaendelea kwa kusuasua lakini mradi wa nguruwe ulisimama baada ya kupata ugonjwa wa homa ya nguruwe na kufa wote.

Alisema shirika hilo pia linatarajia kuanzisha shule ya msingi na kuimarisha bwawa la samaki ambalo litaanza kuvunwa karibuni.

Awali Askofu Libena aliwasilisha salamu za Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Policarp Kadinali Pengo kwa UWAKA kukubali kuwa walenzi wa Masista Wadogo.

Askofu Libena katika mahubiri yake aliwataka wakristu kutafakari upya tabia iliyoibuka kwa kasi sasa ya watu wengi kuwapeleka shule za bweni watoto wenye umri wa miaka miwili kwa kuwa kufanya hivyo kunawakosesha kupata malezi bora ya baba na mama.

Alisema watoto wa umri huo hawawezi kuingia kwenye miito ya usista na Upadre kwa sababu hakutakuwa na maadili ya kumpenda Mungu kutokana na mazingira waliolelewa.

Mwenyekiti wa UWAKA Bw.Dismas Kachemu, alisema toka waanze kusaidia shirika hilo wanaume wameanza kuona umuhimu wa kuchangia hivyo aliwataka wengine ambao hawajatoa michango yao kufanya hivyo.

Katibu wa UWAKA, Bw. Julius Kasonzo, alisema UWAKA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa Parokia zote 67 za Jimbo Kuu Kuu la Dar es Salaam kwa kushirikiana katika kazi za kulijenga Kanisa.

No comments:

Post a Comment