20 July 2011

Wabunge washauri siasa vyuoni zipigwe marufuku

Na Gladness Mboma, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, imeshauri serikali kupiga marufuku viongozi wote wa vyama vya kisiasa kufanya mikutano ya kisiasa katika vyuo vya
elimu ya juu, ili maeneo hayo yatumike kwa shughuli  za mafunzo na utafiti pekee.
 
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati, Bi. Margret Sitta, alisema mbali na hilo, ni vema serikali itafiti vyanzo vya migomo na migogoro katika vyuo vya elimu ya juu vya serikali.
 
Akizungumzia mikopo, Bi.Sitta alisema ili serikali iweze kuimarisha suala hilo, inapaswa kutafuta mbinu mbadala za kupata fedha kuinua uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaoongezeka mwaka hadi mwaka.
 
Alisema wakati wa kutoa mikopo, vigezo maalum vitumike kuwatambua walengwa wenye uhitaji ambao ni wanafunzi kutoka familia zenye kipato duni.
 
“Ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa tangu  mwaka 2006, kiundwe chombo mahususi chini ya bodi ya mikopo kufuatilia  ukusanywaji wa marejesho ya mikopo iliyokwishatolewa.
 
“Aidha, taarifa za mikopo husika zitambulike  kwa walengwa ili kurahisisha ukusanyaji wa fedha hizo kwa ushirikiano wa mwajiri na bodi ya mikopo,” alisema.
 
Alieleza pamoja na hayo, fedha za marejesho ya mikopo hiyo  na matumizi yake zitambulike bayana kwa kuonekana katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wizara kila mwaka wa fedha.

Wakati huo huo Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw.Joseph Mbilinyi,(CHADEMA) amesema chama hicho kitaendelea
kufanya maandamano ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kuendelea  kugoma kutokana na serikali kushindwa kuwatimizia mahitaji yao.
 
Akichangia mjadala wa hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi jana Bw. Mbilinyi maarufu kwa jina la (Mr Sugu) alisema hali hiyo itaendelea kuwepo kwa kuwa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimuya Juu imeshindwa kuondoa kasoro zinazojitokeza.
 
“Maandamano ni poa na yanaruhusiwa, hivyo ruksa wanafunzi kuandama. Nashangaa baadhi ya waheshimiwa tena wamo humu ndani walikuwa wakipinga maandamano lakini juzi walikwenda Mbeya kufanya maamdamano wakiwa wameambatana na waasisi wa CCJ,” alisema.

Bw. Mbilinyi alisema kuwa hata wao CHADEMA wataendelea kufanya maandamano ya amani kwa kuwa CCM nao juzi wakiwa mjini Mbeya walifanya maandamano wakati walikuwa wakiyabeza.
 
Akizungumzia malimbikizo ya walimu,Bw. Mbilinyi alisema  Mbeya kuna walimu 300 wanaodai malimbikizo ya zaidi y sh. milioni 400 na kumtaka Waziri wa Elimu, Dkt. Shukuru Kawambwa, kumweleza ni lini walimu hao watalipwa pamoja na kuitaka serikali kurudisha elimu bure nchini.

Naye mbunge wa Viti Maalum,Bibi. Chiku Abwao (CHADEMA), alisema suala la maandamano ni silaha muhimu katika kufanikisha masuala mbalimbali nchini, kwani bila kufanya hivyo hakuna kitakachoendelea.

“Walimu nchini ndio kielelezo cha umasikini, wanabembeleza kupata haki zao…tunasema maandamano hatayaisha na CHADEMA tutaandamana kwa ajili yao,” alisema.

2 comments:

  1. MAANDAMANO NA MIKUTANO INAYOFANYWA NA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU HAYANUFAISHI CCM TENA. KWA HIYO NI VEMA SERIKALI IYAPIGE MARUFUKU. UNAJUA KULE VYUONI NDIO KUNA VIJANA WENYE AKILI NA UELEWA MPANA WA KUCHAMBUA MAMBO NA AMBAO CCM HAIWATAKI KWA KUWA VIJANA NAO HAWAITAKI CCM. CCM NI WAOVU MNOOOOOO!

    ReplyDelete
  2. PIA WANANIACHA HOI TANZANIA NI WAALIMU, HASA WA PRIMARY SCHOOL. WANAMINYWA HAKI ZAO MNO, MAISHA NI MAGUMU KWAO MNO, MISHAHARA DUNI, MAZINGIRA MAGUMU KWELIKWELI KWAO NA FAMILIA ZAO, HAWALIPWI KWA MUDA LAKINI WAO NDIO WAKO MBELE KUISAIDIA SERIKALI KUWAGANDAMIZA. SIJUI WAMELOGWA?? HALAFU WAO NDIO WANAOFUNDISHA WANAFUNZI. WALIMU NYIE JESHI BWANA TUMIENI AKILI ZENU NA WINGI WENU KUPINGA UOVU WA SERIKALI YA CCM>

    ReplyDelete