20 July 2011

Posho ya wanafunzi elimu ya juu yaongezwa

Na Gladness Mboma,Dodoma
 
SERIKALI imeongeza kiwango cha posho kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka sh. 5,000 za awali, hadi kufikia sh. 7,500 katika mwaka huu wa fedha 2011/2012.Hayo
yalisemwa jana mjini Dodoma Bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa alipokuwa akisoma Makadirio na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2011/2012 kwa wizara hiyo.
 
Dkt. Kawambwa alisema pamoja na ongezeko hilo la posho, pia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itatoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo,na kwa wanafunzi wanaosoma shahada za
uzamili na uzamivu.
 
Alisema kuwa wataimarisha utoaji na urejeshaji mikopo kwa kuoainisha taarifa za wakopeshwaji na zile za Tume ya Vyuo Vikuu na Baraza la Mitihani na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za utoaji wa mikopo karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za kanda visiwani Zanzibar.
 
Dkt. Kawambwa alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitadahili wanafunzi 7,260, ambapo 5,030 ni wa shahada ya kwanza, na 2,230 ni washahada ya uzamili  na uzamivu.
 
“Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam kimedahili wanafunzi wenye sifa za kujiunga na masomo 1,200 kati yao 200 ni wa fani ya sayansi katika
mwaka 2011/2012 ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya maabara, samani za maktaba  na vitabu zaidi vya kufundishia,”alisema.
 
Alitaja mambo mengine yatakayotekelezwa ni kushirikiana na vyuo vya ndani na nje yanchi katika utafiti na mafunzo, hasa kwa shahada za uzamili na uzamivu, ikiwa ni pamoja na kujenga kutoa huduma za afya.

Dkt. Kawambwa alisema mambo mengine yatakayotekelezwa ni pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka 880 hadi kufikia 950 kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
 
Alisema pia wataanza ujenzi wa jengo la utawala, kuendelea kuimarisha na kupanua miundombinu ya kufundishia pamoja na  kujifunzia chuoni hapo.

Aliongeza kuwa wizara itaendelea kugharamia masomo ya wahadhiri katika viwango vya shahada za uzamili na uzamivu.
 
Dkt.  Kawambwa alisema kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine SUA) kitadahili wanachuo 8,572 wa shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya chuo.

“Tutaanzisha shahada mpya saba za kwanza na za tatu za uzamili, kuanza mradi wa uvunaji maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuanzisha taasisi ya kitaifa ya Bioteknolojia ya kilimo ili kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa “Kilimo Kwanza” na kufanya utafiti unaolenga katika kumwondolea mkulima umaskini, kukuza uchumi na kuboresha mazingira,”alisema.
 
Alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 Idara ya Utawala na Rasilimali Watu itaimarisha usimamizi wa utoaji huduma bora za elimu kwa kuajiri watumishi wapya.

1 comment:

  1. nosense, 2500 is nothing, hivi hii 7,500 ni kwa ajili ya nini, naomba nifahamu breakdown (matumizi) ya hizo hela. it is a shame

    ReplyDelete