20 July 2011

TBL yahitimisha mashindano ya pool

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager kwa kushirikiana na Chama cha Pool Tanzania (TAPA), jana ilihitimisha mashindano ya
Safari Lager National Pool Championship 2011, ngazi ya mikoa baada ya kumalizika mwishoni mwa wiki katika mikoa ya Manyara, Mbeya, Mwanza na Kinondoni.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa TAPA Amos Kafwinga, alisema mashindano hayo yalianza Juni 31 mwaka huu hadi Jumapili kwa ngazi za mikoa na kushirikisha klabu 14.

Alisema mashindano hayo, yamemaliza kwa kila mkoa washindi kupata zawadi kama zilivyopangwa.

"Tunapenda kuwashukuru wadhamini wetu bia ya Safari Lager kwa kuweza kufanikisha ngwe hii muhimu ya ngazi ya mikoa kwa ufanisi wa hali ya juu, kwa kweli chama na wachezaji wa mchezo wa pool Tanzania, wanajivunia udhamini huu," alisema.

Naye Meneja wa Safari Oscar Shelukindo, akitangaza zawadi za ngazi ya taifa mwaka huu alisema kampuni yake kupitia bia ya Safari Lager, imekuwa mdhamini mkuu wa mchezo wa pool hapa nchini, na imeweza kuleta mapinduzi ya kweli katika mchezo huo.

Alisema bia ya Safari dhamira yake ni kuendelea kudhamini mashindano ya taifa na mengi mengineyo ya mchezo wa pool nchini.

Pia aliwapongeza viongozi na wachezaji wote kwa kuweza kufanikisha mashindano hayo katika ngazi ya mikoa ambapo alisema inatia moyo kuendelea kudhamini mchezo huo.

No comments:

Post a Comment