20 July 2011

TFF yazipa masharti Simba, Yanga

*Dida kuibukia Mtibwa Sugar

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa masharti kwa klabu za Simba na Yanga, kuwasilisha rasmi maombi ya kuwatoa wachezaji wake
kwa mkopo kabla ya kufika saa sita usiku wa leo vinginevyo wataendelea kubaki nao.

Muda huo ndiyo mwisho wa kufunga dirisha la usajili la uhamisho wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, ambapo baada ya hapo klabu italazimika kusubiri mpaka dirisha dogo Novemba Mosi, mwaka huu.

Yanga imewatoa Omega Seme na Idd Mbaga kuchezea Africa Lyon na Simba ikiwatoa Mohamed Banka (Villa Squad), Juma Jabu (Moro United) na Meshack Abel (Ruvu Shooting) na wengine zaidi ya saba lakini hao watatu wa Simba waligoma kwenda katika timu hizo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema kuna matatizo mbalimbali yalijitokeza katika uhamisho wa msimu na kubwa zaidi lile la wachezaji wa Simba, kugoma kwenda katika timu walizopangiwa kwa mkopo.

"Kesho (leo) saa sita za usiku ndiyo mwisho wa suala hilo, hivyo kama kweli kuna timu ambayo imemuombea mchezaji fulani kwenda timu nyingine kwa mkopo ndiyo zitaonekana kwa kuwasilisha kwa barua rasmi.

"Timu nyingi zimeleta uhamisho wake huku zikionekana zimefanya hivyo, ili kwenda na muda uliopangwa lakini baada ya muda uliopangwa ndiyo utajua ukweli nani kaenda wapi kwa mkopo," alisema.

Alisema mvutano huo unatokana kwa kuwa mtu husika ambaye ni kocha au mtu mwingine wa benchi la ufundi kushindwa kutangaza kitu hicho, kwa vyovyote kocha lazima atatoa sababu za kufanya hivyo lakini timu za nchini hazifanyi hivyo.

"Endapo kama kocha angekuwa ndiye anayetangaza wachezaji wanaotolewa kwa mkopo, sidhani kama wangebisha kutokana na kocha ndiye anayejua matatizo yake na ndiyo maana anamtoa lakini hapa kwetu viongozi ndiyo wanaofanya shughuli hiyo kitu ambacho ni kinyume," alisema Wambura.

Aliziomba klabu kusoma kanuni, ili kuepusha usumbufu unaojitokeza mara kwa mara kwani kila kitu kipo wazi na kusisitiza maombi hayo lazima yawepo makubaliano ya pande tatu.

Wakati huohuo, Wambura alisema wachezaji wa kigeni 'Maproo' walioombewa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), bado wanasubiri majibu kutoka kwa klabu husika na pia kipa wa zamani wa Simba, Deogratius Munishi 'Dida' naye anasubiria kuruhusiwa na timu yake ya Uarabuni kujiunga na Mtibwa Sugar.

"Dida naye aliombewa na Mtibwa Sugar, hivyo uhamisho wake pia unasubiriwa kutoka huko Uarabuni na kwamba mpaka Ijumaa kila kitu kuhusu Maproo kitakuwa tayari," alisema Wambura.

Baadhi ya wachezaji wanaosubiri ITC ni Felix Sunzu, Fernand Onassis Kemo, Hamis Kiiza na wachezaji wengine wawili kutoka Toto African na African Lyon wao wana mmoja.

1 comment:

  1. Hili ni tatizo la viongozi wa Simba na Yanga kujiusisha na usajili wa wachezaji badala ya kocha.Baada ya ligi kuu kuisha kila timu ilikuwa na muda wa kutosha sana wa kufanya usajili pamoja kutoa maamuzi ya wachezaji wanaoachwa na wanaosajiliwa.Ni jambo la kushangaza sana kutoka katika hizi timu mbili zinangoja hadi atua ya mwisho kabisa ya usajili ndipo wanapotoa maamuzi ya sio na msingi kabisa.TFF shikilieni msimamo wenu kama mlivyo amua na kama hizo timu mbili hazitatekeleza wanacho alekezwa basi wabakie na wachezaji wao,na wasubiri usajili wa dirisha dogo baada ya ligi kufikia katikati ya mbio zake.Hili litakuwa fundisho kwa kila timu katika ligi kuu.Simba na Yanga kwa upande mwingine ni timu zinazo changia sana kuuwa vipaji vya wachezaji hapa nchini.Haiwezekani ukawa na timu nzuri yenye wachezaji wanao elewana kama kila mwaka unasajili karibu nusu ya timu na matokeo yake kila wakitia mguu katika mashindano makubwa huishia katika raundi ya pili tu tena kwa bahati sana kutegemea na timu wanazocheza nazo.Viongozi wa Simba na Yanga endesheni timu kama watu walioenda shule.

    ReplyDelete