22 July 2011

Takukuru yachunguza vijisent vya Chenge

Edmund Mihale na Reuben Kagaruki, Arusha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU) imekamilisha uchunguzi dhidi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Jimbo la
Bariadi Magharibi, Bw. Andrew Chenge kwa kuwa na fedha ambazo kama Mtanzania wa kawaida hakutakiwa kuwa nazo.

Pia taasisi hiyo inafanya uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Kagoda ambayo ilihusika kuchota fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alisema tayari jalada la uchunguzi huo dhidi ya Bw. Chenge limewasilishwa menzani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.

Hayo yalisemwa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hoseah, wakati akitoa mada kwenye mafunzo kwa wahariri wa habari kuhusu wajibu wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa.

Alisema suala la kampuni ya Kagoda lina sura mbili, ambapo kwanza iliundwa kamati ya kuchunguza kampuni hiyo. Lakini pia wakati kamati hiyo ikifanya kazi yake, Rais Jakaya Kikwete alihutubia bunge na kuwataka wale wote waliochukua fedha kutoka kwenye kaunti ya EPA, kuzirejesha, kwa ahadi kuwa wale watakaofanya hivyo hawatachukuliwa hatua sheria.

Kamati hiyo kazi yake ilikamilika na kukabidhi ripoti kwa rais na kuhusu mkuu wa nchi ya kutaka waliochukua fedha hizo kuzirejesha, Dkt. Hoseah alisema zilirejeshwa na yeye alishuhudia Manji (Yusuf) akirejesha sh. bilioni 40.

Alisema kazi ya pili ni vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutaka waliohusika na Kampuni ya Kagoda washtakiwe. "Na sisi hatuwezi kukaa kimya, sasa tunachunguza," alisema na kuongeza; "Uchunguzi wa Kagoda unaendelea na wale wenye taarifa kamili waje tushirikiane."

Huku akionekana kujiamini zaidi, Dkt. Hosea alisema; "Rostam Aziz ni nani! Nani anamuogopa Rostam? Tuleteeni ushahidi muone kama hatutamfikisha mahakamani."

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa amekuwa akifanya kazi kwa maelekezo ya rais, Dkt. Hoseah alisema, "Sifanyi kazi kwa sababu Mheshimiwa Kikwete anataka nifanye anavyotaka...mimi nafuata sheria, bosi wangu (Rais Kikwete) hataki rushwa."

Alizidi kusisitiza kuwa; "Tutachunguza tuhuma zote hata Jairo (David) tunamchunguza, nimefanya hivyo bila maelekezo ya rais, mmeniuliza nikasema tunamchunguza, sikusema hebu tusubiri uamuzi wa rais kama alivyosema Waziri Mkuu."  "Sifanyi kazi kwa sababu rais kasema...mimi sikuomba kazi," alisema.

Akizungumzia zaidi suala hilo la Kagoda, alisema wakati wa uchunguzi wa kamati, kwenye taarifa za benki kuhusu wakurugenzi walikuta picha za watu waliokufa. "Zile taarifa za Benki ya CRDB tulikuta picha za watu waliokufa, hebu nikuulize utashughulika na watu waliokufa?"

Alikiri kuwa mtu anayeshiriki vitendo vya rushwa kubwa hatumii akili za kawaida.

Akizungumzia zaidi suala zima la Bw. Chenge, alisema taasisi yake imemchunguza kutokana na kumiliki fedha nyingi, lakini kwenye sakata la rada hakuhusika.

"Chenge tumemchunguza na jalada limepelekwa kwa DPP kuhusu vijisenti...tunamchunguza kwa kuwa na fedha ambazo Mtanzania wa kawaida hakutakiwa kuwa nazo," alisema.

Kuhusu kesi za uchaguzi, Dkt. Hoseah alisema; "Watu wengi watafikishwa mahakamani...sasa tuna kesi nyingi na zitazidi kuwa nyingi, zilianza 10 sasa tunazo 18 na zitazidi kuongezeka."

Akizungumzia kesi ya David Mwakalebela, alisema nayo itarudishwa mahakamani. "Yupo yule tena wa Iringa (Joseph Mungai) na yeye atarudishwa mahakamani," alisema Dkt. Hoseah.

Kuhusu kazi iliyofanywa na TAKUKURU wakati wa uchaguzi hasa kwa kuwakamata kwa tuhuma za rushwa wagombea wengi wa CCM, alisema  anajivunia kazi hiyo hasa kwa kuzingatia kuwa chama hicho ni kikubwa.

"Ningekamata CHADEMA leo hii ingekuwaje! Jambo kubwa ninalojivunia ni kuwakamata CCM, ningetaka kuwashika CHADEMA wasifike hatua tatu, bado mgesema nawaonea."

Kuhusu sakata la wabunge aliokuwa akiwachunguza kwa tuhuma za kupokea posho mara mbili, alisema; "Bado kesi za posho mbili ninazo, sijazifunga bado."  

Alieleza wazi kuridhishwa na kazi iliyofanywa na TAKUKURU chini ya uongozi wake ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa, kazi ambayo alisema haikufanywa kwa maagizo ya rais.

Alisema mtu akitaka kujua utendaji wa TAKUKURU afuatilie kesi zilizopo mahakamani. Alisema tangu uhuru hadi wakati wa utawala wa Mwinyi (Ali Hassan) kesi rushwa ilikuwa moja, wakati wa mkapa moja au mbili, lakini katika kipindi hiki kesi za rushwa kubwa ambazo zimefikishwa mahakamani ni 24.

"Tunasema tukipeleka kesi mahakamani tuna uhakika, tuna ushahidi, hata DPP anapata shida kubwa sana, ana kesi zetu nyingi, sisi ndiyo wateja wake wakubwa sana," alisema
Dkt. Hoseah.

4 comments:

  1. Jamani kwanini hawa watu wanatufanya wananchi kama matahira tusioweza kufikiri. Hosea ameshatuambia kwamba huyo Msukuma mwenzake hana hatia yoyote. Leo anatuambia atamchunguza. Atamchunguzia nini wakati ameshasema hana hatia. Huu si usanii tu. Watu kama Hosea ni wakupuuza because these guys have lost their credibility altogether. Just ignore them. We are tired of that kind of jazz.

    ReplyDelete
  2. Kama Mtanzania jadili hoja kama ilivyo, unapohusisha mambo ya ukabila hapa unapotosha,jitahidi pia kujua sheria kidogo usiwe unajadili kimbumbu.

    ReplyDelete
  3. Kila mtu ana mwenzake. Mimi nina mwenzangu. Wewe una mwenzako.Mzaramo ana mwenzake. Mchaga ana mwenzake.Mhaya ana mwenzake.Mzanaki ana mwenzake. Mkatoliki ana mwenzake.Mwisilamu ana mwenzake n.k. Hata Chenge ana mwenzake. Usitumie Ukabila au Udini kujenga hoja yako.Kubali kwamba Mmasai ni Mmasai kwanza, halafu ni Mtazania. Kwani Mmasai mwingine anaweza kuwa Mkenya!!

    ReplyDelete
  4. Haya tusubiri ya kutoka kwa mzee wa vijisenti na wakati hosea mwenyewe anasema si jambo la kawaida kwa mfanyakazi wa serikali kuwa na akaunti kubwa kama hiyo.
    sasa tujiulize maswali hizo fedha alizipata wapi?na kwa biashara gani anayofanya huyo mzee wa vijisenti.Hata mtu anaye miliki Kagoda anajulikana lakini mambo yanafunikwafunikwa tu.Wewe Hosea unafuata amri kutoka juu wala usitudanganye ya kuwa maamuzi huwa unayatoa wewe mwenyewe na ukiambiwa huwa kuna watu unawaogopa unakataa lakini huo ndio ukweli wa mambo.Kuna tabia ya viongozi wa kitanzania ya kukataa kuwajibika hata kama jambo linaoneka liko wazi kabisa.Kwa mtazamo huu hii nchi haita badilika siku zote.

    ReplyDelete