20 July 2011

Upinzani wataka elimu ya msingi iwe miaka 9

Na Gladness Mboma, Dodoma

KAMBI ya Upinzani Bungeni imeishauri serikali kuongeza muda wa elimu ya shule ya msingi kutoka miaka saba ya sasa hadi kufikia miaka tisa au kumi.Mbali na hilo, imeshauri
mfumo wa elimu ya sekondari ufanyiwe mabadiliko kutoka miaka sita ya sasa kuwa miaka minne kwa kuunganisha mitaala ya vidato vya tatu, nne,tano na sita kuwa mtaala mmoja wa elimu ya sekondari.

Mapendekezo hayo yalitolewa na Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Christowaja Mtinda, wakati akiwasilisha bajeti ya upinzani kwa wizara hiyo kwa mwaka wa 2011/2012.

Alisema ikiwa utaratibu  huo utakubaliwa watoto watamaliza shule wakiwa na umri wa miaka 15 na 17, umri unaomwezesha kijana kukaribia kuanza maisha ya kazi.

“Utaratibu huu utaenda sambamba na mpango unaoendelea wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhuisha mfumo wa mitaala ili iweze kufanana, hivyo kuwa na elimu inayofanana  na  hadi sasa ripoti ya awali imeshawasilishwa wizarani,”alisema.

Bi.Mtinda alisema kambi hiyo imeshauri mitaala ya elimu ya msingi upanuliwe kwa kuingiza muhtasari wa kidato cha kwanza na cha pili.

Alisema kuwa mtaala huo ukipanuliwa utawapatia vijana wa kike stadi za kuweza kujikinga na tatizo la kuanza ngono katika umri mdogo , hivyo kupunguza au kumaliza
kabisa tatizo la mimba za utotoni.

Kambi hiyo ilipendekeza utoaji wa chakula cha mchana mashuleni ili kukabiliana na wimbi la utoro na tabia ya wanafunzi kusinzia darasani.

Kwa upande wa elimu ya sekondari alisema Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005/2010  na ya mwaka 2010/2015 ilitamka wazi kuwa serikali itajenga vyuo vya VETA kwa kila wilaya nchini, lakini cha kushangaza ni kuwa ahadi hiyo mpaka sasa bado
haijatekelezwa.

No comments:

Post a Comment