26 July 2011

Mancini azozana na Balotelli

LONG BEACH, California

KOCHA Roberto Mancini amezozana tena na mshambuliaji wake Mario Balotelli, wakati alipomtoa katika mechi ya kirafiki kati ya Manchester City dhidi ya
LA Galaxy.

Kocha wa City alimtoa uwanjani Balotelli, baada ya kukosa bao akiwa na kipa akitaka kufunga kwa mbwembwe kwa kisigino.

Kwa bahati mbaya mpira ulipaa juu ya goli, Mancini alikasirika na kuruka juu na kumwamuru James Milner kusimama na kufanya mazoezi kabla ya kuchukua nafasi ya Balotelli dakika chache baadaye.

Mambo yalikuwa mabaya wakati Balotelli alipomhoji kocha wake kuhusu uamuzi aliochukua, kitu kilichofanya wapigiane kelele kwenye mstari wa kutokea mbele ya mashabiki wa kimarekani.

Baada ya mechi hiyo iliyomalizika sare ya bao 1-1, kabla ya City kushindwa kwa penalti 7-6, Mancini  alisema: "Kila wakati tunahitaji kuwa makini katika kazi yetu, na katika wakati huo sidhani kama Mario alifanya hilo. Ndiyo maana nilimtoa nje.

"Anajua alifanya makosa. Katika soka kila wakati unatakiwa kuwa makini na kama unapata nafasi ya kufunga, unatakiwa kufunga. Ninatumaini atakuwa amejifuza kwa hili. 

"Ni adhabu inayomtosha kwa kutolewa baada ya kucheza dakika 30. Na kwangu hilo sasa limekwisha.

“Mario ni kijana. Lakini kila wakati ninataka kumsaidia. Kama akiwa makini, anaweza kucheza kwa dakika 90, asipofanya hivyo, atakuwa katika benchi, na hiyo ni kwa wachezaji wote."

Alipoulizwa ni kitu gani Balotelli alimjibu wakati akitoke uwanjani, Mancini alisema: "Tulikuwa tukiongea kitaliano. Kwa kingereza itakuwa ngumu kukuambia tafsiri yake. Lakini, Mario ni mtoto wa mjini, anajua hakuotea."

Kocha wa Galaxy, Bruce Arena  alisema: "Ninafikiri ilikuwa ni kituko. Sijui ni kitu gani mchezaji alikuwa akifikiria, pengine alifikiri kuwa aliotea na kushindwa kufunga bao,” alisema.

Mancini amekuwa akimuunga mkono Balotelli ambaye ana vituko tangu aliposainiwa City kwa ada ya pauni milioni 23, mwaka jana.

City ilipata bao lake kipindi cha kwanza katika Uwanja wa Galaxy wa Home Depot Center, ambapo David Beckham aliichezea timu hiyo.

Balotelli aliifungia timu yake kwa mkwaju wa penalti, kabla ya kutolewa.

Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa City, na ilikuwa chupuchupu kupoteza mechi.

Mchezaji wa Galaxy aliyetokea benchi Mike Magee, aliisawazisha dakika ya 54, Beckham ambaye katika mechi hiyo alicheza dakika zote, alikosa nafasi kadhaa za kufunga.

Baaada ya dakika 90 kumalizika, timu hizo zilipigiana penalti, ambapo City ilishinda mabao 7-6, kipa wa City, Joe Hart, ndiye aliyefunga bao la ushindi.

Wakati huohuo, mchezaji Yaya Toure amesema kuwa, Machaster City inaweza kuwa Barcelona nyingine kwa uchezaji wake, licha ya kuwa timu hizo mbili ni tofauti.

Barcelona ni moja ya timu nzuri zaidi duniani kwa muda mrefu sasa, na timu nyingine zimekuwa zikijaribu kucheza vizuri.

No comments:

Post a Comment