26 July 2011

TBF yaiomba serikali kuwajibu

Na Addolph Bruno

SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF),  limeiomba serikali kuwajibu mapema maombi yao kuhusu kukarabatiwa Uwanja wa Ndani wa Taifa ili waweze
kujipanga mapema kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Kanda ya Tano yatakayofanyika baadae mwaka huu.

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kanda ya Yano ya mpira wa kikapu yatakayoanza Oktoba mwaka huu kwa kuzishirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu wa Rais wa TBF, Phares Magesa, alisema wanaomba kupata uhakika wa marekebisho ya uwanja huo kutokana na ukubwa wa mashindano na kwamba, shirikisho halina fedha.

"Mambo yanaendelea kufanyika kwa kiwango kidogo, lakini bado tuna mambo mengi, tumepelekea barua wizarani, tukiomba kututekelezea maombi yetu mapema," alisema Magesa.

Alisema mashindano hayo ambayo yatashirikisha timu za wanawake na wanaume, yanatakuwa kufanyika kwenye uwanja wa ndani kama wenye viwango vya kimataifa kama ilivyo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali na hilo, TBF kupitia kiongozi huyo imewaomba wadau na kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano hayo yanayohitaji zaidi ya sh. milioni 200.

"Kuna gharama mbalimbali kama malazi, usafiri wa ndani, posho za waamuzi na mambo mengine mengi yanayohitaji fedha, hatuwezi kufanikisha bila msaada wa watanzania," alisema.

Alisema Tanzania itawakilishwa na klabu nne ambazo ni Savio na KBC kwa upande wa wanaume,  huku wanawake ni JKT na Jeshi Stars.

No comments:

Post a Comment