21 July 2011

Guardiola amtamani Sanchez kuliko Fabregas

BARCELONA, Hispania

KOCHA wa timu ya Barcelona, Pep Guardiola ameripotiwa kutaka kumsainisha mshambuliaji raia wa Chile, Alexis Sanchez lakini kasema pia wanafanya majadiliano na
kiungo wa  Arsenal, Cesc Fabregas.

“Tunahitaji mshambuliaji. Tuna wachezaji wengi zaidi kwenye nafasi ya kiungo kuliko safu ya ushambuliaji,” alisema Guardiola kwenye mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari, tangu alipotwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya katika Uwanja wa Wembley mapema mwaka huu.

“Bojan Krkic na Jeffren Suarez, wote wanataka kuondoka hivyo washambuliaji ni muhimu sana,” aliongeza kocha huyo.

Wakati Barcelona msimu uliopita ilikuwa ikitesa katika kuwania ubingwa, lakini inaonekana msimu huu huenda ikapata upinzani mkubwa kutoka kwa Real Madrid, ambayo msimu uliopita iliboresha benchi lake.

“Idadi ya mechi kwenye kalenda inatisha,” alisema Guardiola, ambaye timu yake imeongeza michuano ya Kombe la Dunia kwa klabu katika michuano yake ya ligi ya nyumbani na Ulaya msimu huu.

Guardiola alibainisha kuwa uchezaji wa Sanchez, unarandana na mfumo wa Barcelona ambayo inahitaji mshambuliaji ambaye anabadilisha nafasi, ili kuweza kutoa pasi fupifupi.

No comments:

Post a Comment