26 May 2011

Chanjo yaua ng'ombe 22 Geita yaathiri 278

Na Faida Muyomba, Geita

NG’OMBE 22 wanadaiwa kufa ambapo wengine 278 wameathirika baada ya kupatiwa chanjo ya homa ya mapafu katika Tarafa ya Butundwe,wilayani Geita hivyo
wamiliki wa mifugo hiyo wametishia kuishitaki serikali.

Akizungumza na wanadishi wa habari ofisini kwake ,Daktari wa Mifigo Wilaya ya Geita, Dkt. Thobias Kiputa,alikiri kuwepo kwa tatizo hilo.

Alisema tayari,timu maalumu ya wataalamu kutoka wilayani wamepelekwa katika tarafa hiyo kushirikiana na wataalamu wa kata kwa lengo la kuhakikisha wanalipatia ufumbuzi wa kina ikiwa ni pamoja na kuwapa matibabu ng’ombe waliopatwa na matatizo hayo.

"Hali hiyo ni ya kawaida kutokea pale chanjo inapokuwa inafanyika yakiwa ni matokeo hasi baada ya chanjo lakini chanjo kama chanjo haiuwi.Na ukiangalia idadi ya ng’ombe tuliowapatia chanjo katika Tarafa ya Butundwe pekee ni 26,043 ambapo wanaodaiwa kufa ni 22 tu na 278 wakiwa wamepatwa na hali hiyo ya matokeo hasi,’’alisema.

Alisema, matokeo hasi yanapotokea kwa ng’ombe aliyepata chanjo ya ugonjwa huo, ni lazima taarifa zitolewe haraka ili  kutibu jeraha kwa wakati muafa huku akiwatupia lawama baadhi ya wafugaji kuwa ni wazembe kufuatilia pindi tatizo linapotokea.

Alisema kuwa mifugo Wilaya ya Geita, sababu nyingine iliyochangiwa kuwepo kwa hali hiyo ni kutokuwepo kwa chanjo ya aina hiyo katika wilaya hiyo  yenye ng’ombe zaidi ya 500,000 katika kipindi cha miaka 8 kwa kuwa hapakuwa na daktari.

Kwa upande wao ,baadhi ya wafugaji wa Kijiji cha Kageye, ambako ng’ombe 11 wamedaiwa kufa na wengine 58 kuathirika baada ya kupatiwa chanjo hiyo,wamedai kuwa huenda dawa hiyo ilikuwa imepitwa na wakati.

Baadhi ya wafugaji wakiwemo Bw. Tono Sloloja na Bw. Silvesta Samson wamedai kuwa iwapo hawatapata majibu ya kuridhisha watakwenda mahakamani kuishtaki serikali ili kuwalipa fidia mifugo hiyo  mara baada ya kupatiwa chanjo hiyo.

No comments:

Post a Comment