08 April 2011

Warioba: Wananchi wasizibwe midomo

*Ni katika mjadala wa Muswada wa Katiba mpya
*Ataka kila kitu kijadiliwe kupata kwa uwazi
*CCT yasema rais amepora madaraka ya wananchi


Na Tumaini Makene

PAMOJA na kuzuka kwa zogo kubwa lililosababisha mkutano wa utoaji maoni ya Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Katiba kuvunjika, muswada huo umeendelea kukosolewa kwa kiasi kikubwa, huku serikali ikiambiwa isizibe watu midomo, kuhoji au kuzungumza baadhi ya masuala 'kwani hayo yanayozuiliwa kuhojiwa ndiyo katiba yenyewe'.

Imeelezwa kuwa itakuwa si sahihi kuwazuia Watanzania kuhoji baadhi ya masuala ya msingi hata kama tayari yapo katika katiba ya sasa, kwani ni bora yakajadiliwa kwa kina ili yajulikane kama yanakidhi mahitaji ya watu kujitawala au la.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na mmoja wa viongozi waandamizi wastaafu nchini, Jaji Joseph Warioba, wakati akitoa maoni yake katika kuboresha muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba, akisisitiza kuwa masuala yaliyoko sehemu ya 3, kifungu cha 9(2), yajadiliwe bila zuio lolote.

Kifungu hicho cha muswada, kinataja mambo 8 ambayo ni marufuku watu kuyahoji au kuyazungumzia wakati tume ya kukusanya maoni ya watu juu ya katiba mpya itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake.

Masuala hayo yanayoitwa kuwa ya 'heshima na utukufu', hivyo hayapaswi kuguswa kwa maslahi ya taifa, yameainishwa katika muswada kama ifuatavyo; Kuwepo kwa Muungano wa Tanzania na Zanzibar, kuwepo kwa mihimili mitatu ya dola (bunge, serikali na mahakama), nafasi ya urais, mshikamano wa kitaifa na amani ya nchi.

Mengine ni; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwepo kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, haki za binadamu, dhana ya utu wa mtu, usawa mbele ya sheria na mfumo unaoweka utaratibu wa kufuata sheria, dhana ya Serikali ya Tanzania kutokuwa na dini na uhuru wa mahakama.

"Haya mambo yanayoitwa matakatifu na hivyo hayaguswi ndiyo katiba yenyewe, ndiyo mambo ya muhimu katika katiba huwezi kuyaondoa watu wasiyazungumze...lazima watu wayazungumze hata kama tayari yako katika katiba ya sasa. Msiwazuie watu kusema, kama ni muungano tuwaruhusu waseme.

"Watu wasikilizwe, wengine hawafurahishwi na muundo wa muungano ulivyo sasa, wengine watataka serikali moja, wengine serikali tatu, kama wakiweza kuwashawishi watu wengi wasikilizeni, hata kama watasema hatutaki kuwa na rais waache waseme, wanataka kuzungumzia Serikali ya Mapinduzi waacheni, huu ni wakati wa masuala haya kujadiliwa, maana ndiyo yanayozungumzwa sana sasa, ndiyo katiba haya.

Jaji Warioba ambaye mbali ya kuwahi kuwa jaji wa mahakama kuu pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema kuwa kifungu hicho kifanyiwe marekebisho kisiwazuie Watanzania kujadili mwafaka wa kitaifa juu ya mstakabali wa taifa lao.

Jaji Warioba pia alionekana kushangazwa na vyama vya siasa na asasi zingine za kiraia kuzuiwa kuelimisha wananchi kwa kufanya kampeni wakati wa upigaji kura ya maoni ya 'ndiyo' au 'hapana' ili kupitisha sheria ya kuanza kutumika katiba mpya, badala yake shughuli hiyo kusimamiwa na tume ya uchaguzi.

Huku akionya Watanzania kuacha ushabiki katika suala la utungaji wa katiba mpya, Jaji Warioba alisema "sasa mimi najiuliza hii tume itakwenda kufanya kampeni juu ya nini, tume iliyohusika katika mchakato wa katiba kweli inaweza kwenda kuwaambia wananchi wapige kura ya ndiyo au hapana. Waachwe watu wafanye kampeni.

"Kama ni vyama vya siasa au watu waacheni wapige kampeni. Lakini natoa angalizo hili si jambo la ushabiki, huu ni mwafaka wa kitaifa. Tusifanye ushabiki, tutafute mantiki," alisema Jaji Warioba, huku akishangiliwa baada ya mwanzoni kuonja zomea zomea, alipoonekana akisifia baadhi ya vipengele katika muswada huo.

"Pia hapa imeelezwa kuwa baada ya bunge la katiba kupitisha rasmu ya katiba, rais atatia saini, sasa kwa kawaida bunge la katiba likishapitisha kitu hakuna tena assent ya rais. Halafu baada ya rais kutia saini mnataka iende kwa wananchi, sasa sheria inapitishwa halafu inakwenda kwa wananchi, je, wakiikataa itakuwaje."

Jaji Warioba alishauri kuchaguliwa kwa njia mojawapo kati ya bunge la katiba au mkutano jumuiko la kitaifa la katiba, huku pia akitoa angalizo juu ya kura ya maoni kuangalia namna ya kuratibu kura za pande mbili za muungano.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alikuwa mchangiaji wa tatu baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema kuwa ni vyema serikali ikaweka wazi juu ya jina la muswada huo, kwani wananchi wanazungumzia utungwaji wa katiba mpya, si marekebisho ya katiba.

Alisema kuwa ni vyema muswada huo ukabeba dhana sahihi kwa ajili ya mabadiliko ya katiba kwani kinyume chake, kitasababisha hata vifungu vya muswada huo kuwa vibovu, huku akitoa angalizo kuwa si sahihi muswada huo kutoa mamlaka makubwa kwa rais, kwani mamlaka ya kuongoza nchi yanapaswa kutoka kwa wananchi.

Alisema kuwa katiba inazaa taasisi zote, ikiwemo ya urais, hivyo Watanzania wanapaswa kuzungumzia masuala yote, bila kuzuiwa, huku akitaka baadhi ya maneno yaliyomo katika muswada huo yafafanuliwe vizuri ili yasitumike kuminya haki za Watanzania katika tafsiri zake.

"Hiki kifungu cha 9(2) kinachosema mambo yasiyogusika, si kwamba Watanzania hawataki muungano, anayesema kuwa hataki muungano huyo ana matatizo yake, lakini Watanzania wanachotaka ni kuzungumzia aina gani ya muungano, wanahoji madaraka ya Tanganyika yako wapi, maana kumekuwa hakuna clarity katika suala la muungano.

"Si kwamba hawataki rais awepo, wanahitaji kujadili urais wa namna gani, maana hapa kuna suala limechakachuliwa, tumechukua mfumo wa Marekani na Uingereza, sasa wanataka kujua tuko upande upi, tusianze kuweka limit (vizuizi) katika kujadili katiba, maana hapa tunatengeneza nchi yetu si nchi ya mtu mmoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa kama mchakato wa uandikaji wa katiba mpya utaanza vibaya, nchi inaweza kuingia katika matatizo makubwa ya kisiasa, hivyo ni vyema mchakato huo ukapata uhalali wa kisiasa kutoka kwa wananchi, badala ya mamlaka makubwa kuachiwa rais.

Akisisitiza suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili na jina la muswada huo kubadilishwa, kutoka kusomeka marekebisho ya katiba, bali uandikwe Muswada wa Utungaji wa Katiba mpya, Prof. Lipumba alisema kuwa wananchi hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia mchakato wa kura ya maoni kwani inaweza kuzichakachua.

"Karibu kila kitu kinatokana na rais hapa, mapendekezo yatokane na wananchi, si rais. Tukianza hivyo itakuwa mwanzo mbovu, ili mchakato huu upate uhalali ni bora utokane na wananchi, msimpatie rais mzigo mkubwa kiasi kwamba mambo yakiharibika aonekane yeye ndiyo kaharibu. Katika kura ya maoni hatuna imani kabisa na tume ya uchaguzi.

"Hatuna imani nayo kabisa maana tume hii mwaka jana katika uchaguzi mkuu ilituchakachua kweli kweli, sasa hawa hawa tena wanapewa kazi ya kusimamia kura za maoni, matokeo yatakuwa tayari yanajulikana, tunataka tume inayoaminiwa na watu. Kuwepo na nia thabiti, maana tukianza vibaya tutaingia katika matatizo makubwa ya kisiasa," alisema Prof. Lipumba.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia alisema kuwa muswada huo haujatungwa kwa nia njema, akitaka umma upatiwe nafasi kubwa ya kuamua namna ya kujitawala, si mamlaka hayo kuwekwa mikononi mwa rais kwa kuamua mchakato mzima utakavyokwenda, huku naye akisisitiza suala la jina la muswada huo libadilishwe, usomeke kuwa ni 'katiba mpya'.

"Hatutaki damu imwagike lakini serikali inaweza kuchochea vurugu, hatutaki katiba ya CCM, tunataka katiba ya wananchi, rais hapa anapewa madaraka yote. Pia lazima tuwe makini hapa maana tuna complex state maana tuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tofauti na nchi kama Kenya ambao wana simple state, maana ni Jamhuri ya Kenya," alisema Bw. Mbatia.

Zamu hiyo ya wawakilishi wa makundi mbalimbali iliendelea mpaka kufikia kwa Chama cha APP- Maendeleo na Chama cha Walemavu nchini, ambaye alitaka kundi hilo kuzingatiwa na kupewa umuhimu mkubwa unaostahili katika mchakato mzima mpaka kupatikana kwa katiba mpya, akitoa angalizo kuwa kwa sasa muswada umewaweka pembeni na kuwasahau.

Ilipofika zamu ya mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda, Bw. Tambwe Hizza, ambaye mara muda mfupi baada ya kuwasilisha hoja yake, yalianza kusikika makofi yasiyokoma yakipigwa na baadhi ya wahudhuriaji, ikiwa ni dalili ya kuzomea, huku yeye akipuuza kwa kusema "Mwenyekiti hayo tulishayazoea, yaache."

Katika hoja yake ambayo ilikuwa ikikatishwa mara kwa mara kutokana na zomea zomea hiyo, hatimaye ilizua mtafaruku wa kambi mbili zinazopingana na kusababisha mkutano huo kuahirishwa kwa muda, Bw. Hizza alisema kuwa iwapo mchakato wa katiba mpya hautafuata sheria zilizopo na katiba iliyopo, nchi haitapata katiba mpya, badala yake itaambulia vurugu.

Alisema kuwa si sahihi wananchi kutaka kumnyang'anya rais mamlaka yake katika mkutano kama huo wa utoaji maoni ya muswada, kwani mamlaka aliyonayo yamewekwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, akisema kuwa ibara ya 98 ya katiba ya sasa, inaruhusu katiba kubadilishwa au kufutwa kabisa.

Zomea zomea, zilizoanza kwa makofi yasiyo na mwisho, hatimaye kupigwa miguu chini na kibwagizo cha 'atokeeee atoke, aondokeeee aondoke, ilizidi na kumlazimisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Bi. Pindi Chana kuahirisha mkutano kwa ajili ya chakula, kisha uanze baadaye.

Hata hivyo aliporudi baada ya kusimama kwa mkutano huo takribani saa mbili, Bi. Chana alisema haiwezekani kuendelea, bali mkutano huo wa kuchukua maoni utaendelea leo kwa watoaji kuwasilisha kwa maandishi na wengine wataruhusiwa kuzungumza.

Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu alisema kuwa zomea zomea hiyo ni suala la aibu, kwani kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake na wengine wanapaswa kusikiliza hata kama hawataki au hawaungi mkono maoni hayo. Aliongeza kuwa hali hiyo ikiendelea muswada utapitishwa bungeni bila wananchi kutumia fursa hiyo ya kuujadili na kuuboresha.

CCT yaonya rais kupora madaraka ya wananchi

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeonya serikali kuwa kitendo cha rais kuteua tume kukusanya maoni ya katiba mpya ni kuwapokonya wananchi haki zao kwamba lengo la kazi hiyo haitafikiwa.

Pia imesema serikali isithubutu kuharakisha suala hilo kulenga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuongeza kuwa iwapo watanzania hawatapata muda wa kutosha kutoa maoni yao kwa uhuru itakuwa haijakidhi matakwa ya watanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Makamu wa kwanza wa Mwenyekiti wa CCT, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dkt. Valentino Mokiwa, jumuiya hiyo imesema mwenye mamlaka ya kuteua tume hiyo ni bunge kwa niaba ya wananchi na si rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala.

"Ipo hatari ya kukasimu mamlaka haya kwa Mheshimiwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Tawala kuteua Tume ya kusimamia mchakato huu ikiwemo sekretarieti yake.

"Ni sharti wananchi wenyewe wawezeshwe kutoa maoni yao moja kwa moja au kwa njia ya wawakilishi wa makundi yote ya kijamii, alisema Askofu Mokiwa katika taarifa hiyo na kuongeza.

"Utaratibu huu unamfanya Rais awe wa mwanzo na mwisho (Alpha na Omega) na kuondoa ushiriki wazi wa wananchi katika kusimamia na kuamua mstakabali wa nchi yao. Ni vyema mamlaka haya yakakasimiwa na wawakilishi wa wananchi kupitia bunge na vyama vya siasa," alisema Askofu Mokiwa katika taarifa hiyo.

Alisema Watanzania wanahitaji katiba mpya ili kukidhi matakwa yao ambayo hayajawai kufikiwa na marekebisho yaliyokuwa yakifanyika katika katiba ya sasa, chini ya mfumo huo bila kuleta faida.

Katika barua hiyo iliyoelekezwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Celina Kombani yeye kichwa cha habari, tahadhari kutoka CCT juu ya muswada wa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2011, CCT iliikumbusha serikali kuwa wananchi ndio wenye maamuzi ya mwisho juu ya nchi yao na si rais.

"Tunakuomba utumie weledi na hekima yako kuhakikisha kwamba rai yetu inapewa nafasi na umuhimu katika jambo hili, ili kuleta umoja, usawa, amani na utangamano pamoja na maendeleo ya nchi yetu yatakayotokana na katiba iliyoandaliwa na wananchi wenyewe," alisema.

CCT ilisema katiba ijayo inatarajiwa kukidhi haja ya kizazi cha leo, kesho na kijacho na si kama marekebisho yaliyopita ambayo hayakukidhi haja ya Watanzania.

"Muswada unafifisha na kudhoofisha ari na matarajio yao, mabadiliko yamekuwa yakifanyika kila mara lakini bado lengo la kupata katiba mpya halijakidhiwa," alisema Askofu Dkt. Mokiwa.

13 comments:

  1. Tafadhali kumbukeni kuwa wananchi ndio wanamuweka hata rais madarakani, kwa hiyo ndio wenye nchi, budi washirikishwe kikamilifu katika suala hili. Hayo mambo matukufu yatabakiza utukufu wake ikiwa wananchi wanaridhia iwe hivyo na si kulazimishwa iwe hivyo. Kumbukeni leo ni CCM kesho anaweza kuwa mwingine, hivyo katiba isitungwe kwa kukidhi haja ya chama au kundi fulani kwani ni ya wote. Hakuna ajuaye kesho na kesho kutwa. Ikitungwa vibaya itaumiza waliopo na wajao.

    ReplyDelete
  2. huu ndo mwanzo wa uharibifu wa amani,na serikali ndo inataka kuharibu, wangefanya research ktk nchi zilizowahi kutokuwa na amani. wataona mazingira tuliyonayo kwa sasa yalichangia kiasi kikubwa ktk uvunjifu wa amani.

    ReplyDelete
  3. Hatuhitaji Marekebisho ya Katibu maana Katiba hii ya Kizazi cha Nyerere Kilichopita. unahitaji KATIBA MPYA. Itakayoendana na mahitaji ya Kizazi hiki. Tafadhali serikali msitutungia katiba kama hadithi za kibibi kizee. Tunahitaji Katiba Mpya. Tambwe acha propaganda za kipuzi laana ya Mungu itakushukia.

    ReplyDelete
  4. Wapendwa Wana wa Tanzania wenzangu, nina maswali machache tu kuhusu swala la Katiba mpya. Pamoja na kukubali kwangu ya kwamba Katiba mpya ni muhimu kwa sasa ninaogopa ya kwamba mambo yanaweza kwenda bila uhakika. Hapa nina maswali machache kwa wachangiaji wa hoja hii: 1. Je nikwamba Watanzania hawajapewa nafasi ya kutoa mawazo yao hadi sasa? Mbona naona kuna mijadala mbalimbali inayofanyika nchini? Baba Mpendwa Askofu Mokiwa na CCT je ni kweli ya kwamba Rais wa nchi yetu hawakilishi Watanzania wote kwa uteuzi wa Tume hii. Iwapo sisi ndio tuliompa utumishi huu je kuna ubaya gani iwapo yeye atatenda jambo kwa niaba yetu? Nina hakika ya kwamba yeye hutamka kwa niaba ya wote na bila shaka kabla ya kutamka huwa amepata mawazo na mahusia toka kwa watu mbali mbali wakiwemo viongozi. Ombi langu ni hili; Rais wetu asaidiwe na wote, ili atoapo jambo lisiwe lake; na kama atafanya kinyume chake hivyo basi alaumiwe na kukosolewa.

    ReplyDelete
  5. Ninacho ona hivi sasai kwamba viongozi wa chama tawala wameshalewa madaraka na wanataka kuwaburuza watu.Wananchi wanatakiwa vilele kutowa maoni yao.kwa sababu wao ndio wako mitaani kila siku na kuona mambo yanavyo kwenda.Itakuwa sio haki kabisa ya kusema ya kuwa raisi ndio atoe kauli ya mwisho ya katiba iwe vipi.Haya ndio mambo yanayotokea leo hii huko Tunisia,Egypt na kwingineko,Kama kweli ccm imedhamiria kuondoa machafuko nchini basi haina budi kusikiliza wananchi wake badala ya kiongozi moja kusimama na kusema hiyo haiwezekani na hayo ni mawazo ya watu kumi.Je watu hao ni akina nani?,Labda angeulizwa alafu afafanue hiyo kauli yake.Hivi kweli tunaviongozi ambao wanawezakukaa chini na kujiuliza kama wanachofanya kiko sawa au hakikosawa?

    ReplyDelete
  6. Mtoa maoni wa nne kutoka juu nashukuru kwa maoni yako yakistaarabu sana. Swali ulilomuuliza askofu Mokiwa linaweza kujibiwa na yeyote siyo lazoma Mokiwa mwenyewe. Naomba nikujibu kama ifuatavyo:-
    1. Ni kweli kuwa watanzania bado hawajapewa nafasi ya kutoa maoni kuhusu katiba mpya maana ndio sasa muswada wa mchakato wa katiba unatarajiwa kupelekwa bungeni. Muswada huu unahusu ni jinsi gani watu watatoa maoni yao katika tume ya kukusanya maoni ya katiba. Muswada huu una mapungufu mengi kwani unataja kuwa ni marekebisho ya katiba na siyo utungwaji katiba mpya. Pia muswada umeweka limit katika mambo ya msingi ambayo ndio katiba yenyewe yasizungumziwe katika katiba hiyo inayotarajiwa kurekebishwa au kuandikwa upya.
    2. Katika suala la katiba rais kamwe hawezi kuwa mwakilishi wa wananchi. Hapa hata bunge ambalo wajumbe wake ni wawakilishi wa wananchi nalo halina nafasi ya kuwatungia wananchi katiba. Hii inatokana na ukweli kuwa katiba ni mkataba wa wananchi jinsi wanavyotaka nchi yao itawaliwe namna gani, anayewatawala afanye nini na siyo rais awatungie watu katiba. Rais, serikali na wabunge na mamlaka ya mihimili mingine yapo kwa mujibu wa katiba iliyotungwa na wananchi. Katiba yetu ya sasa ilitungwa na wakoloni na wananchi sasa baada ya kujitawala miaka 50 na kupata weledi wa kutosha sasa tunataka kujitungia katiba yetu inayoendana na Tanzania ya sasa na si vinginevyo.
    3. Kwa kuweka limit baadhi ya mambo kama madaraka ya Rais, Muungano, Masuala ya uchaguzi, na mengineyo kuwa ni matakatifu yasizungumziwe ni ishara tosha kuwa serikali haina nia njema ya kutunga katiba mpya bali inatekeleza wajibu tu. Hii ni wazi kuwa maneno ya akina Kombani na Werema sasa yamejidhihirisha kuwa hawataki katiba mpya. Hii inaweza kusababisha amani kunjika na tukiwaruhusu wapumbavu kama akina Tambwe basi tutaweka rehani nchi yetu na amani itatoweka na hapa wa kulaumu atakuwa ni serikali.
    4. Kwa maoni yangu ni kwa Rais kwa kuwa ni mwenyekiti wa Chama cha sisa na kwa kuzingatia kuwa alichaguliwa kwa kura nyingi lakini wapo wananchi zaidi ya milioni 2 ambao walimktaa, haistahili apewe madaraka ya kuunda tume ya maoni ya mchakato wa katiba kwa vile ataendesha mambo hayo kwa kuzingatia ushauri na kanuni za chama chake hivyo hatawatendea haki wadau wengine wa vyama vya siasa. Pili tume ambayo ataunda kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar ni lazima ataipa hadidu za rejea kuwa wafanye yale ambayo atataka kama ilivyo tume ya uchaguzi ya sasa ambayo huagizwa ni lazima Rais wa CCM ashinde. Tatu, mambo yaliyokatazwa yasizungumziwe ndio hasa katiba yenyewe. Kwa mfano hamtaki watu wazungumzie muungano wala madara ya Rais kuna nini hapa? Wananchi tunataka katiba ambayo tutampa Rais majukumu ya kufanya akiwa ikulu, siyo kwenda kutalii ughaibuni wala kuteua vidosho na mamis kuwa wakuu wa wilaya au mikoa. Rais apangiwe ni namna gani atawapata watumishi wake amam wa serikali. si katiba ya sasa inayomruhusu Rais kuteua hata shemeji zake kushika madara makubwa ya kitaalamu wakati hawana uwezi wala taluma. Tunataka katiba itakayomuwajibisha Rais akizembea kwa mambo ya msingi kama ya Richmond, dowans, n.k
    5. Watanzania tuache ushabiki wa akina Werema na Kombani na wengine wanaofanana na hao maana ni wapumbavu hawa waliolewa madaraka haya ya muda. Rais kama ameamua kweli kwa moyo mkunjufu kuandika katiba mpya basi aruhusu mjadala wa uhuru kusiwe na vikwazo kama wanavyoleta sasa.
    Mwisho nawaonya kuwa CCM na serikali wsipoangalia watangamiza nchi hii kwa suala hili la katiba. Naona walidandia hoja za wapinzani za kuandika katiba mpya bila kufanyia utafiti wa kutosha. Katiaka hili la katiba jikazeni kama wanaume ili watanzania waandike katiba yao hata kama haitawapendelea nyie mtatafuta mbinu ingine ya kujiimarisha zaidi bila ya kutegemea katiba hii ya sasa ambayo inawanufaisha kwa asilimia mia. Huu ni wakati wa CCM kutahiriwa bila ganzi acheni kulia maana nje ya boma la kutahiria kuna wanawake watawasikia mkilia kitu ambacho kwa mwanaume ni aibu. Nia aibu kubwa chama dola kama hiki kuchakachua hata muswada wa katiba.

    ReplyDelete
  7. eng.mwakapango,E.P.AApril 9, 2011 at 11:15 AM

    suala la katiba linagusa maisha ya watanzania wote ikiwa ni pamoja na ustawi wa nchi. nchi takribani zote zenye ustawi na maendeleo duniani ni kutokana na katiba nzuri zilizotungwa kwa kufuata maoni na matakwa ya wananchi. mimi najiuliza Rais Jakaya Mlisho Kikwete anao washauri wazuri kweli inawezekana washauri alionao wamemsaliti na hawamtakii maisha mema. lazima tufike mahali tumsaidie Rais wetu anaweza kuwa ameingiliwa na al shabab kwenye utawala wake. ushauri mwingi kwake una utata mkubwa kwa wasomi kuna haja gani ya kumshauri rais madudu ifikie watu kupigwa mabomu wakati wa kwenda kutoa maoni yanayohusu katiba yao? CCM lazima ifahamu kilicho na mwanzo kina mwisho huu ndio umefika mwisho tujipange upya lakini tusiwe kikwazo cha kuleta maisha mapya ya watanzania kwa kuwa na mfumo mzuri wa kidemokrasia unaoana na Katiba. maoni yaliyotolewa CCT yaangaliwe kwa karibu yanawakilisha watu wengi. namheshimu Jaji Joseph Warioba alichosema ni cha msingi serikali iache uoga acha wananchi watoe dukuduku zao.

    ReplyDelete
  8. Rais Kikwete afahamu kuwa kwa maamuzi yeke yasiyo sahihi yakutaka kuanza rafu mwanzo wa mjadala huu.Wananchi watanzania hawatakaa kimya na kuendelea kuona hali kama tulikotoka ikiendelea kutokea. Nguvu ya umma itatumika kudai haki yawaliowengi, madhara yote yatakayotokea yatakuwa ni juu yake.Hatuko tiyari kuona kikundi kidogo kikiendelea kuwakoromea nakuwandesha. watanzania kama kitakavyo. Wacha watanzania wajadili kila kitu kuhusu nchi yao na si kuwapangia ni kipi cha kujadili na kipi cha kuacha.Huo utakatifu wa baadhi ya mambo yasiyotakiwa kuguswa ni kwaniaba ya watanzania wote au hicho kikundi kidogo kinachojineemesha na kitakachojineemesha na katiba ijayo?

    ReplyDelete
  9. Wanaoleta fujo kwenye mswada wa katiba mpya ni CCM kwani wanajua watakosa ulaji! Na bado mtaukosa sana!

    ReplyDelete
  10. TUNAHITAJI KATIBA MPYA,HATUHITAJI KUTAJIANA AL SHABAB AU KUONGOZWA NA AMRI KUMI ZA MUNGU (KANISA) NI UJINGA KUTIA MAMBO YA KIJINGA KAMA HAYA,WAPO WAJINGA WENGINE UGANDA WANAMSUMBUA MUSEVENI KWA KUTAKA UGANDA IONGOZWE NA AMRI KUMI ZA MUNGU NA TANZANIA HILO LIPO KWA UJANJA UJANJA,HUU NI USHAMBA NA KUWA NA WATU AMBAO BADO BADO WANADHANI WANALALA NA NG'OMBE NA MBUZI NDANI YA MABANDA NDIO MAANA KILA WAKIJADILI KATIBA UTAWASIKIA WANAINGIZA MAMBO YA KIDINI NDANI,KWANI HUYO MWANASHERIA MKUU NI MUISLAMU? WAPUMBAVU NYIE

    ReplyDelete
  11. Mtoa maneno hapo juu, sijui ana mwelekeo gani katika kuifundisha jumuiya yetu. Kwa maneno yake hayo yalijaa maneno machafu hayanisaidii mimi. Ninaamini Watanzania wanapenda na kutarajia kuwepo na Katiba mpya. Swali linakuja namna ya kuiunda upya Katiba hii: Wananchi raia na Wazalendo wana haki ya kuchangia jambo hili kwa kina na wala si kwa ghadhabu ya kumchukia mtu mmoja au Chama fulani. Bila shaka kwa kupitia vikao halali basi tutapata maoni sahihi. Ikumbukwe ya kwamba Watanzania sasa tumezidi milioni 40. Je mawazo ya watau milioni arobaini yatafikishwaje kwenye utekelezaji. Hapo basi wanahitajika wawakilishi wetu. Amri kumi za Mungu anazozitaja jamaa hapo juu hazina uhusiano na utungaji wa Katiba yetu bali zinahusiana na Sheria hata za kimahakama; kama vile Usiibe, Usiue, Usitamani cha mwenzio na kujichukulia kikawa chako, ukifanya hivyo na kuvunja sheria basi utahukumiwa. Soma vizuri chanzo cha Sheria ili kutenganisha mambo. Mimi pia sikubaliani na Udini ua Ukabila au chochote kihusucho kumbagua mtu. Hekima inahitajika katika mambo yote.

    ReplyDelete
  12. Jamani huu ni muswada wa kutunga katiba mpya tuelewe kwanza,inabidi upitishwe bungeni ndio mchakato uhalalishwe kuanza, na hapo ndio hiyo kamati itateuliwa. sio kelele tuu hata hiyo Kamati haijaundwa,na hata huu muswada haujapitishwa na wananchi watapewa fursa ya kuchangia kwa miezi zaidi ya 6 sio kitu cha mara moja na msifanye watu hawana fikra kama zenu na katiba ikishajadiliwa itarudi sasa bungeni kule ndio hao wawakilishi wetu wataijadili kwa kina kutokana na mawazo na fikra zetu tuwe Makini, nashangaa linavaliwa njuga na hao wanasiasa kulifanya ni lao wakati hili ni letu wananchi

    ReplyDelete
  13. Mi, naona kuwa Watu tumekosa busara katika hili! Kwa nini, kwa sababu sikutegemea wasomi wa tanzania ya leo, wangejadili Muswaada huu kwa jazba! Hivi jazba au misisimko ndo mjadala au Mjadala unaendehwa na hoja? Ifike mahali wasomi wetu wanaotuongoza kujadili Muswaada huu watumie hoja na si kelele kwani mwisho wa siku hatutafika mahali tunapotaka kwenda, vilevle naomba nitoe wito huu, Chadema nana CCM wasitumie Mswaada huu kutufanya tufarakane sisi watanzania! Wapeleke hoja kwani Mswaada huu ni wa watanzania wa itikadi zote awe mwanachama na asiye Mwanachama kwani si watanzania wote wana ushabiki wa vyama, hivyo naomba mijadala hii isiongozwe kwa maslahi ya vyama bali kwa maslahi ya watanzania wote.

    ReplyDelete