Na Dunstan Bahai
SERIKALI imewatupia lawama wafanyabiashara nchini kwa kusababisha kupanda kwa bei ya vyakula kutokana na kukificha kilichopo kusubiri hali ya
ukame ili kupandisha bei.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Christopher Chiza wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Bw. Chiza alikuwa akifafanua jambo juu ya Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri wa Kilimo wa nchi wanachama wa Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu uliofanyika Februari 24 na 25 mwaka huu Makao Makuu Ndola, Zambia.
Alisema Tanzania inajitosheleza kwa chakula na hata bei za vyakula zilizopo hazistahili kwa kuwa zipo ziada ya tani 1, 176, 076.
Bw. Chiza alisema Tanzania inahitaji tani milioni 11.1 za chakula lakini kwa msimu wa mwaka jana imefanikiwa kuvuna tani 12,322,161.
“Tathmini iliyofanywa na wizara imegundua chakula ni kingi sana kwani tuna ziada kubwa tu. Bei imepanda ya vyakula kutokana na wafanyabiashara kuvificha wakisubiri ukame ili wapandishe zaidi bei,” alisema.
Alisema kwa sasa serikali inashindwa kuwadhibiti wafanyabiashara hao ikiwa ni pamoja na kushindwa kutoa bei elekezi kutokana na kutokuwepo kwa chombo cha kusimamia mazao hayo ya chakula.
“Tumezindua bodi itakayosimamia mazao mchanganyiko yakiwemo ya nafaka ambayo ndiyo itasimamia na kudhibiti mfumuko wa bei. Kwa sasa tunazo bodi za mazao ya biashara tu kama vile sukari, pamba, korosho na mengineyo,” alisema.
Alisema kwa sasa nchi haina njaa kwani ipo mikoa kama ya Kigoma na Nyanda za Juu Kusini wakulima wanaendelea kuvuna.
Akizungumzia mkutano huo wa alisema wamekubaliana nchi wanachama kutoa michango yao haraka iwezekanavyo ili wadudu hao wanapoibuka kudhibitiwa.
Alisema kama serikali imetoa ruzuku ya pembejeo ya sh. bilioni 148, itakuwa haina maana kama wadudu hao wataibuka nakula mazao ya wakulima.
Bw. Chiza alisema wadudu hao huzalishwa zaidi Tanzania katika Bonde ya Igunga,Mto Maragarasi, Katavi na Bahi na kwamba Tanzania inatakiwa kulipa ada ya uwanachama ya dola za Marekani 185,120.
Nchi nyingine wanachama ni Kenya, Malawi, Zimbabwe, Msumbiji na Zambia na kwamba miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ni kuzishawishi nchi za Afrika Kusini, Lesotho, Swaziland, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga.
“Hawa wadudu hawahitaji paspoti wala viza, wakizalishwa wanakwenda popote, hawana mipaka,” alisema Bw. Chiza.
Nani awakemee kama si serikali ya CCM?
ReplyDeleteNdio waliowaweka madarakani ninyi sio, si wananchi.
Kwa hiyo kwa vile mnawaogopa, mnaanza kulalamika, ili tuwaonee huruma au mnataka tuwachukie wafanya biashara?
Serikali isiyo na meno haiachi kulalamika na kutoa sababu lukuki.
Inaona bora iwakabili CHADEMA kuliko kuwakabili mafisadi.