04 March 2011

Migodi kuguswa balaa la umeme

*Kamati ya Bunge yataka ipunguziwe matumizi
*Yadai wanatumia umeme kibao, hawana mgawo


Na Mwandishi Wetu

WAKATI suluhisho la mgawo wa umeme nchini halijapatikana huku suala la ama kuwasha au kutowasha mitambo ya Dowans likisumbua
vichwa vya Watanzania, imefahamika kuwa Kamati ya Bunge ya Bunge ya Nishati na Madini imependekeza yafanyika mazungumzo na migodi ya madini ili kuona kama inaweza kupunguza matumizi ya nishati hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Januari Makamba alisema jana kuwa migodi hiyo imekuwa ikitumia umeme mkubwa unaofikia megawati 125 kila mmoja, lakini haikuwahi kukumbwa na mgawo wa umeme, jambo ambalo wamesema likikubaliwa sehemu ya nishati hiyo inaweza kusambazwa kupunguza makali katika maeneo mengine.

"Migodi inatumia umeme mwingi sana na haikatiwi hata siku moja, kila mgodi unatumia megawati 125 kwa siku kwa migodi minne ni umeme mwingi sana, tumeshauri kuwepo kwa mazungumzo ya kupunguza matumizi ya umeme kwenye migodi kwa kipindi hiki," alisema Bw. Makamba.

Hilo ni moja ya mapendekezo makubwa manne ya upatikanaji wa umeme haraka ili kupunguza makali yaliyotolewa na kamati hiyo, likiwamo la kuwasha mitambo ya Dowans, ambalo hata hivyo linaweza kuathiriwa na kesi iliyopo mahakamani.

Akizungumzia suala hilo, Bw. Makamba alisema hakuna mahakama iliyozuia utekelezaji wa mapendekezo yao kuhusu hatua za dharura kunusuru nchi na janga la ukosefu wa umeme kama ilivyodaiwa bali kilichozungumzwa ni kwamba serikali itatakiwa kutoa taarifa yoyote iwapo kuna hatua za mazungumzo juu ya matumizi ya mitambo ya Dowans au suala lolote nje ya chombo hicho.

"Tuliwauliza mawakili wa TANESCO kilichosemwa na jaji ni kuwa kama kuna mazungumzo nje ya mahakama basi taarifa itolewe ili mahakama isimamishe kwanza shauri, haijazuia mapendekezo yetu jamani," alisema Bw. Makamba.

"Lakini pia hata kama tungeachana na hilo la mitambo ya Dowans bado kuna mapendekezo mengine matatu ambayo ni muhimu sana kufanyiwa kazi na serikali," alisema Bw. Makamba.

Pendekezo jingine ni pamoja na serikali kuwashwa mitambo ya IPTL yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 kwa siku ambayo kwa sasa inazalisha megawati 10 tu.

Pia waliishauri TANESCO ifanye marekebisho kwenye transfoma zake, umeme unaopotea kwa siku ni sawa na asilimia 75 ya umeme wote unaozalishwa na Songas kwa mwaka mzima ili kuokoa kiasi hicho.

1 comment:

  1. Mtawaambiaje wapunguze matumizi ya umeme wakati mliwavutia wenyewe na kuwaambia umeme upo tena mkawapunguzia na gharama. Acheni unafiki we Makamba mdogo, tatizo si MIGODI HAPO, migodi inamatatizo kwenye mikataba. Tatizo la umeme ni serikali kiziwi, DOWANS/RICHMOND,na kina ROSTAM. Mnazunguka kula allowance tu.

    ReplyDelete