07 March 2011

Barcelona yazidi kuchanja mbuga

BARCELONA, Hispania

BAO lililofungwa kipindi cha kwanza na mchezaji Seydou Keita limeifanya Barcelona kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zaragoza.Ushindi huo pia
kunaifanya timu hiyo iendelee kujichimbia kileleni wa ligi, ikiwa mbele kwa pointi 10 dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Real Madrid.

Bao hilo ambalo liliihakikishia ushindi huo, Barcelona lilipatikana dakika mbili kabla ya timu hizo kwenda mapumziko baada ya Keita, kuunganisha pasi aliyotengewa na Lionel Messi.

Hata hivyo timu hiyo ya Catalan, ingeweza kuondoka na ushindi mnono, lakini mlinda mlango wa Zaragoza, Antonio Doblas alikoa mabao mengi kipindi cha kwanza na kuifanya isiadhirike zaidi.

Kwa ushindi huo wa nne mfululizo umeifanya, Barcelona kufikisha mechi 25 bila kufungwa ikiwa ni sawa na rekodi ambayo timu hiyo iliiweka msimu wa mwaka 1973-74.

“Timu ilielewana vizuri na kutawala mchezo,” alisema mchezaji wa Barcelona Xavi Hernandez. “Tulikuwa tukicheza na timu ambayo ilikuwa haitaki kushambulia na ndiyo maana mchezo ukawa mgumu,” aliongeza.

Wakati wa mchezo kocha, Pep Guardiola alikuwepo uwanjani baada ya kuwepo kwa wasiwasi wa kwamba maumivu ya mgongo yanayomkabili, yangweza kumfanya aikose mechi hiyo.

Kocha huyo alikuwa ameungana na wachezaji David Villa na Andres Iniesta kwa ajili ya mechi ya marudiano hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, dhidi ya Arsenal ambayo itafanyika kesho.

Katika mchezo huo, Zaragoza ilipata nafasi pekee dakika ya nane kipindi cha kwanza, baada ya mchezaji, Nicolas Bertolo alipotumia maarifa yake kumpita Gabi Milito, ambaye alicheza mechi hiyo kutokana na Carles Puyol kuwa majeruhi, lakini jitihada zake hizo zikatibuliwa na Gerard Pique.

No comments:

Post a Comment