16 March 2011

Lowassa apeleka watu kunywa dawa

*Akodi gari kila kata kwenda Loliondo
*Babu Mwaisapile arejeshwa kazini KKKT


Na Waandishi Wetu

WAKATI maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Tanzania wakizidi kumiminika kupata dawa kwa Mchungaji Mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwaisapile, Mbunge wa
Monduli, Bw. Edward Lowassa naye ametangaza kujitolea usafiri kupeleka watu jimbo lake Loliondo kupata tiba kwa mchungaji huyo.

Hatua hiyo imekuja wakati taarifa za karibuni zikianza kutoa ushuhuda wa watu mashuhuri na wale wa kawaida kuwa wamepona maradhi sugu yaliyokuwa yakiwasumbua, ukiwamo ukimwi, kisukari, saratani, shinikizo la damu na upungufu wa nguvu za kiume.

Bw. Lowassa aliyewahi kuwa Maziri Mkuu kabla ya kujiuzulu, anakuwa mbunge wa pili kufanya hivyo baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Bw. Phillemon Ndesamburo kujitolea kufanya hivyo.  

Taarifa zilizopatikana wilayani Monduli na kuthibitishwa na Bw. Lowassa, zinaeleza kuwa mbunge huyo alijitolea kuwapeleka watu hao kuanzia juzi, kwa kugharamia usafiri na mambo mengine kama maji ya kunywa.

Mmoja ya watu walipiga simu katika chumba cha habari cha Majira kwa masharti ya kutotajwa jina lake gazetini alisema ameamua kufanya hivyo ili kufikisha ujumbe wa shukrani kwa Bw. Lowassa kwa kitendo hicho.

Alisema Bw. Lowassa ambaye ni mbunge wa jimbo hilo aliamua kufanya hivyo baada ya watu wa jimbo hilo kuwa na nia ya kufika huko lakini hawakuwa na uwezo wa kufanya hivyo kutokana na gharama za usafiri kuwa juu.

Alisema watu wote wamekuwa wakijiandikisha katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na huduma hiyo imekuwa ikitolewa bila kuangalia itikadi za kichama katika kata 10 za Monduli, ingawa hata watu kutoka mjini Arusha walionekana kujiandisha ili kusafiri kwenda kwa 'Babu'.

"Ametoa gari moja kwa kila kata litakalowapeleka wakazi hao kupata dawa, hivi mimi nipo hapa nasubiri zamu yangu," alisema.

Akizungumzia suala hilo, Bw. Lowassa alikiri kufanya hivyo kwa lengo la kuwasadia watakaohitaji kwenda kunywa dawa hiyo.

"Ni kweli nimefanya hivyo kutokana kuwepo kwa vuguvugu la habari za kuwepo kwa mchungaji katika Kijiji cha Samunge kuwa anatoa dawa ya kutibu watu wa maradhi mbalimbali.

"Hivyo nimeamua kuwasadia lakini si pekee yangu, bali nasaidiana na wengine wanachangishana na kukodi magari ili kwenda huko kwa kuwa ni mbali. Jana (juzi) walikwenda watu 100 katika kijiji hicho leo tena (jana) wanandelea kujitokeza kujiandikisha," alisema.

Bw. Lowassa alisema ataendelea kutoa msaada huo kulingana na uwezo wake wa kifedha iwapo utahurusu katika siku zijazo.

Mwaisapile arudishwa kazini

Wakati Babu Mwasapile akizidi kuvuta watu, Kanisa lake la KKKT limemrudisha kazini kwa kumwongezea mkataba wa ajira usiyo na kikomo, ikiwa ni miaka minne baada ya kustaafu, hivyo kumwezesha kuendelea kupata mshahara na stahili zingine.

Ajira hiyo isiyo rasmi imetokea kwa mchungaji huyo mara baada ya kudaiwa kupata karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuanza kutibu magonjwa sugu yakiwemo kisukari, saratani na UKIMWI kwa kile kinachoelezwa kuwa tiba hiyo inafanyika kwa njia ya imani na kimaombi.

Kuajiriwa upya kwa mchungaji huyo kutamwezesha kupata mshahara kama kawaida na kusitisha pensheni aliyokuwa akiipata kama mchungaji mstaafu.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Thomas Laiser alithibitisha kurudi kazini rasmi kwa mchungaji huyo jana, akisema kanisa hilo limetafakari na kubaini umuhimu wa mchungaji huyo katika dayosisi hiyo na taifa kwa ujumla, na kumrudisha ili atumikie umma akiwa ndani ya kanisa hilo.

Alisema mchungaji huyo alipewa kazi hiyo na Mwenyezi Mungu tena kazi kubwa kuliko hata ile aliyokuwa akiifanya kabla ya kustaafu, hivyo iwapo ametukuzwa na Mungu kiasi hicho vipi wao wasimjali na kumweka katika himaya ya kanisa.

Mchungaji Mwaisapile ambaye atabakia katika Usharika cha Sonjo alipokuwa akitumikia awali, alistaafu baada ya kulitumikia kanisa hilo katika maeneo mbalimbali, ukiwamo Ushariki wa Babati Mjini, Mkoa wa Manyara kwa miaka saba kabla ya kuhamia Sonjo alikotumikia kwa miaka 12 hadi kustaafu.

Tumeaona tumweka vizuri ili aweze kutenda kazi aliyotumwa na Mwenyezi Mungu kwa ufanisi zaidi akiwa anajitosheleza kimapato na kwamba mpango huo hauna kikomo…lakini lugha rahisi ndiyo hiyo kwamba ameajiriwa upya,� alisema Askofu Laiser.

Alisema tayari amemwagiza Katibu Mkuu wa KKKT, Bw. Israel Kariyongi
kutekeleza maamuzi hayo yaliyofikiwa na Kanisa Machi 3, mwaka huu wakati timu ya viongozi wa kanisa hilo ilipomtembelea kijijini Samunge na kufikia maamuzi hayo kwa pamoja.

Alisema baada ya mchungaji huyo kuelezwa uamuzi huo aliridhika na maamuzi ya kanisa ukizingatia kuwa hana makuu na kwamba kanisa linaamini kwa kumweka katika mazingira mazuri ya kiuchumi anaweza kufanya kazi hiyo ya Mungu kwa ufanisi mkubwa.

Taarifa zaidi kutoka Samunge zimeeleza kuwa huduma inaendelea kama kawaida lakini usafi hasa wa chupa za maji bado ni tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi kikamilifu.

Mkono wa Babu sasa umekuwa mwepesi kweli kweli, anaweza kufuta gari zaidi ya 20 kwa muda mfupi tu na hiyo naamini inasaidiwa na wagonjwa kufuata utaratibu uliowekwa na serikali kwamba huduma itatolewa katika magari pekee…lakini bado tatizo kubwa lipo
kwenye usafi, hali ni mbaya sana,� alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kampuni mmoja ya uzalishaji soda na maji kupeleka bidha hizo kwa kiasi kikubwa na kuuza kwa bei ya kawaida tayari matumizi ya maji yameongezeka na kusababisha idadi kubwa ya chupa tupu na maji kuzagaa ovyo.

Basi latelekeza wateja wa babu

Basi la Kampuni ya Air Msae jana lilitelekeza abiria 80 waliokuwa wanakwenda kupata tiba kwa babu baada ya kuharibikia eneo la Ngerenaro, kilomita moja kutoka mjini Arusha.

Baada ya tukio hilo, dereva wa gari hilo alitokomea kusikojulikana na baadaye kukamatwa na polisi wakishirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) na kulitoza sh. 250,000 kwa kuendesha gari bovu.

Wakati huo huo, Mzee Piniel King’ori (65) aliyedaiwa kwenye gazeti hili jana kupotea baada ya kunywa dawa Loliondo amegundulika amekufa ikiwa ni siku 11 tangu alipoochana na wenzake.

Mwili wa mzee huyo umepatikana baada ya kufukuliwa baada ya  kuzikwa na wenyeji Tarafa ya Sale wilayani Ngorongoro baada ya
kutotambulika.

Wenzetu waliokwenda Loliondo wametutaarifu kuwa ndugu yetu amefariki na kuzikwa baada ya kutotambulika, hivi tunaendelea na taratibu za msiba huku tukisubiru mwili wake urejeshwa kwa mazishi ya heshima itakavyoamuliwa na vikao vya familia,� alisema Bw. King’ori nyumbani kwa marehemu eneo la Sekei wilayani Arumeru.

11 comments:

  1. Ngastukaaa! Kumbe Dini ni siasa?
    watu wanatoa matamko, wengine wanalaani.
    wengine wanabariki, machale kundesa chunga imani yako, ngastukaa watu hawana Imani?

    ReplyDelete
  2. nawapongeza viongozi wa KKKT kwa uamuzi wa busara wa kumrudisha kazini mchg.
    pia sikufurahishwa na kauli ya mtume Mwingira kwenye gazeti la mwananchi16/03/2011.
    KWA KWELI HEKIMA NA BUSARA ZINAHITAJIKA SANA KATIKA KUTOLEA MATAMKO HII HUDUMA YA MCHG.

    ReplyDelete
  3. kwa nini huyo mzee alifariki na alikuwa anatembea mwnyewe,wala hakuwa mahututi

    ReplyDelete
  4. Taifa limepoteza lengo. Hatuna Viongozi. Tunatawaliwa kwa kuamini Ushirikana.Watawala wetu wanaamini UCHAWI.Si ajabu hao hao walikuwa wanapeleka vidole vya Albino kwa waganga wa kienyeji wakahakikishiwe kama watashinda Ubunge na kuchaguliwa Uwaziri.Sasa Mawaziri. Wabunge n.k. wanapeleka wapigakura wao Loliondo badala ya kujenga hospitali na kuboresha matibabu kwa wananchi! Mungu ibariki Tanzania!!!

    ReplyDelete
  5. Huyu "BABU" inabidi ashitakiwe kwa kudanganya Taifa eti "KAONGEA NA MUNGU NDOTONI". Vile vile hawa akina Lowasa wawe mashahidi katika hiyo kesi kwa kudanganya Wananchi kwa masirahi yao binafsi.Huo ni UFISADI. Wanaendelea kuwanyima wananchi haki zao. Matibabu mazuri haspitalini n.k. Lowasa hata baada ya kunywa kikombe kwa babu, huyoo atakwenda Ulaya kutibiwa.

    ReplyDelete
  6. HE nyie KKKKT hebu acheni unafki huo,miaka yote tangia aondoke kwenu hamjamthamini mnakuja kumthamini leo kisa amekuwa maarufu!hio hela anayopata ndio riziki yake.acheni hizo eti mtamlipa mshahara kumbe sasa imekuwa biashara sio.mwacheni babu atoe huduma kivyake nyie kama mnataka kutoa msaada na toeni tu.watu bwana ukipata umaarufu kidogo utawaona......

    ReplyDelete
  7. Katika maandiko matakatifu tunasoma kuwa Mungu alisema "Mimi ndio njia na atakaye nifuata mimi atakuwa na uzima tele, amina.

    ReplyDelete
  8. Watanzania tuwe na akili wakati huu sio wa kudanganywa ni wakati wa tekinologi tuanglie mambo ya mbele ya kakobe yameishia wapi sialikuwa anatoa mjini watu tuko nyuma bado katika wale matapeli wa bongo huyu mzee ndio kavunja recodi watanznia kaeni chonjo saa mbayaaaa.

    ReplyDelete
  9. Huyu BABU jamani sio mtu wa kawaida tayari keshajiita NABII na anaonana na Mwenyezi Mungu basi nakuambieni huu ni unafiki na ushirikina wa hali ya juuuu kabisa kwa anayemuamini mungu angalieni sana

    ReplyDelete
  10. Wananchi wanasubiri usemi wa Rais kuhusu huu ujinga wa kwenda Loliondo na magari ya serikali. Wafanyakazi wa serikali kuacha kazi kwa siku nyingi wakifuata matibabu ya uongo na kiushirikina. Watanzania tusiwe wajinga kiasi hicho. Umasikini usitufanye wapumbavu. Dunia nzima inatutazama kwa kutushangaa!!

    ReplyDelete
  11. Kama hakuna njia mbadala zilizo wazi na zenye ushahidi wa kisayansi basi dawa ya BABU ndiyo tiba pekee inayokidhi kiu ya wagonjwa waliojikatia tamaa. Hivyo wewe kama HUIAMINI ni bora ukakaa kimya badala ya kutoa kashfa kwani pilpili usiyoila yakuwashia nini?

    ReplyDelete