16 March 2011

Wabunge walia na misamaha ya kodi

Na Tumaini Makene

TAKRIBANI asilimia 94 ya utajiri unaopatikana katika madini unapelekwa nje ya nchi bila kutozwa kodi, kutokana na sheria mbovu zinazoruhusu misamaha ya
kodi iliyokithiri hususan kwa kampuni kubwa katika sekta hiyo.

Halikadhalika kampuni hizo zimekuwa yakifanya ujanja katika kuhakikisha kuwa yanakwepa kodi hasa kwa kutumia mbinu za 'mtaji mdogo' na 'utapeli wa kughushi bei halisi ya vifaa' ambapo Tanzania imeweza kupoteza takribani dola za Marekani milioni 883, ambazo zingeweza kukuswanya kama kodi kutoka kwa wachimba madini hao.

Kutokana na misamaha hiyo ya kodi, Tanzania ndiyo nchi pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ina kiwango kikubwa cha kusamehe kodi, ikiwa ni asilimia 2 kwa pato la taifa, ambapo kwa mwaka wa fedha 2009-2010 pekee, nchi imepoteza takribani sh. bilioni 630.

Fedha hizo zilizopotea katika misamaha ya kodi, ambayo haina umuhimu, iwapo zingesimamiwa vizuri na kuingizwa katika pato la taifa kuinua uchumi wa nchi, zingeweza, kwa mfano, kujenga barabara ya lami kutoka Iringa-Dodoma mpaka Babati au kununua mtambo mpya wa kuzalisha umeme wa megawati 400, hivyo kumaliza kabisa tatizo la nishati hiyo nchini.

Mianya hiyo ya misamaha ya kodi kwa makampuni makubwa, yakiwemo ya madini, ujenzi na mengine, imeelezwa kuwa chanzo cha ukosefu wa mapato kwa serikali, badala yake inaongeza kodi katika maeneo ambayo yanamgusa mlaji moja kwa moja, ilihali moja ya kampuni za madini ikitajwa kuwa itaanza kulipa kodi ya faida ya uzalishaji, mwaka 2019 wakati ilianza uchimbaji tangu mwaka 1999.

Hayo yalisemwa jana katika semina ya wabunge juu ya usimamizi wa bajeti, walipokuwa wakichangia mada kadhaa juu ya ukusanyaji wa mapato ya serikali, ziliyowasilishwa na Mtendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Bw. Placidus Luoga, ambapo wabunge wengi walionekana kulia juu ya urasimu na mianya ya rushwa katika ukusanyaji kodi nchini.

Waliishauri TRA kuhakikisha inafanyia kazi malalamiko ya wateja katika maeneo mbalimbali, hasa kuhusu matatizo ya kuchelewesha makontena Bandari ya Dar es Salaam, hali inayosababisha wateja wengi kuhamia Bandari ya Mombasa, huku nchi ikizidi kukosa mapato ambayo yangeweza kufikia asilimia 80 ya makusanyo ya TRA.

Akizungumza na Majira kando ya semina hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Kabwe Zitto alisema kuwa nchi inapoteza fedha nyingi katika misamaha ya kodi ambazo iwapo zingedhibitiwa, zingeweza kuinua uchumi, kutengeneza ajira kisha kuongeza pato la taifa.

Alisema kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita, Tanzania imesamehe kodi za takribani dola za Marekani milioni 630, "fedha zote hizi zingedhibitiwa tungeweza kujenga barabara ya lami kutoka Iringa, Dodoma mpaka Babati, au kununua mtambo mpya wa kuzalisha umeme wa megawati 400 na kumaliza kabisa tatizo la mgawo nchini.

"Sisi tunaogoza kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na kiwango kikubwa cha asilimia ya misamaha ya kodi, hasa kwa kampuni kubwa za madini na wakandarasi wa sekta ya miundombinu. Lakini pia kama ulivyoona katika mada za watu wa TRA ukusanyaji wa mapato unazidi kupungua.

"Labda hapa nizungumze kama Waziri Kivuli wa Masuala ya Fedha na Uchumi, ukusanyaji wa kodi unapaswa kuchangia asilimia 20 katika pato la taifa, lakini sasa unachangia asilimia 15 tu kama ulivyosikia katika mada za watendaji wa TRA," alisema Bw. Zitto.

Akinukuu taarifa ya Kamati ya Bomani ambayo yeye alikuwa mmoja wa wajumbe, Bw. Zitto alitolea mfano namna kampuni za madini zinavyokwepa kodi kwa ujanja wa 'mitaji mdogo' na 'kughushi gharama za bei halisi', akisema;

Kwa upande wake Mbunge wa Singida Kusini, Bw. Tundu Lissu alisema kuwa TRA hawana kosa, wala wananchi, bali bunge ndilo linastahiki kubebeshwa mzigo wa lawama kwani ndilo mwaka 1997 lilipitisha sheria tatu, alizosema zilileta mabadiliko makubwa katika sekta hiyo, hasa katika misamaha mikubwa, hivyo nchi kupoteza mapato.

"Mtoa mada wa mwisho amesema kitu kikubwa sana lakini kwa sauti ndogo sana amesema kuwa moja ya changamoto kubwa ni excessive tax exemptions...kati ya dhambi kubwa ambayo bunge hili limewahi kufanya ni kutunga sheria hiyo ya misamaha ya kodi. Hapa wa kulaumiwa si TRA, wala Watanzania, ni bunge linapaswa kuwajibika.

"Katika taarifa ya Kamati ya Bomani ya mwaka 2008, ilisema kuwa kwa miaka 10 iliyopita yaani 1998 mpaka mwaka 2007 sekta ya madini imezalisha takribani dola bilioni 829 ambapo kodi zingine pamoja na mrahaba tumepata sh milioni 283 ambayo ni sawa na asilimia 5.8 ya mapato.

No comments:

Post a Comment