16 March 2011

Kikwete aelezwa makali ya mgawo

Na Edmund Mihale

WAZIRI wa Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo amemweleza Rais Jakaya Kikwete jinsi makali ya mgawo wa umeme yanavyoathiri uzalishaji katika sekta ya
uchumi na kijamii nchini.

Akitoa taarifa ya Rais Kikwete alipotembelea wizara hiyo jana, Bw. Mkulo alisema, "Athari kubwa ni kupungua kwa mapato ya ndani kutokana na kushuka kwa uzalishaji. Bajeti ya serikali imebidi kutumika kusaidia ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura," alisema Bw. Mkulo.

Alisema kuwa hali hiyo imesababisha kupanda kwa gharama za maisha kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma.

Sababu nyingine iliyosababisha ugumu wa maisha, alisema kuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia iliyosababishwa na hali mbaya ya kisiasa katika nchi za kiarabu.

Akitoa majumuisho ya taarifa hiyo, Rais Kikwete hakuzungumzia suala hilo bali masuala mengine, huku akiitaja wizara hiyo kuwa moyo wa nchi katika uendeshaji, hivyo inatakiwa kuwa makini katika utendaji wake.

"Wizara ya fedha ni kama moyo kwa binadamu, ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa serikali ikizembea shughuli zote za serikali zinasimama," alisema Rais Kikwete.

Mbali na hilo, alizungumzia Sheria ya Manunuzi ya Umma kuwa ndiyo inayotoa mianya ya rushwa, na kuitaka wizara hiyo kuhakikisha inasimamia eneo hilo kwa umakini makubwa.

Hata hivyo Rais Kikwete alisema pamoja na kuwa sheria hiyo ni nzuri lakini ni ngumu katika utekelezaji, aakaitaka wizara hiyo kuagalia namna inavyoweza kuiboiresha kuwa tija katika jimii.

"Jamani sheria hii ni nzuri lakini ina ugumu wake, nakumbuka nilikwenda Halmashauri ya Mahenge wakanimbia kuwa iwapo watasimamia wao ujenzi nyumba zao watajenga moja kwa sh. milioni 15 lakini wakitumia sheria hiyo watajenga moja kwa sh. milioni 46, hapa mtaona kuwa kuna nyumba tatu kama watasimamia wao.

"Katika sheria hii ndipo watu wanapokula wanaibia serikali sasa hilo mliangalie," alisema.

Rais alizungumzia sheria hiyo wakati kuna mjadala miongoni mwa wabunge kuwa kuna mpango wa kubadili sheria hiyo na kuondoa kifungu kinachozuia kununua bidhaa zilizokwishatumika, ikiwamo mitambo ya Dowans.

Uhamisho wa wafanyakazi

Rais Kikwete aliwataka watendajiwa serikalia kutowahamisha wafanyakazi iwapo ofisi zao hazitakuwa na fedha.

Alisema hali hiyo inachangia kuongezeka kwa deni la serikali na hatimaye kusababisha migomo isiyo na lazima katika sehemu za kazi.

Ukuaji wa uchumi

Rais Kikwetea aliitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa inaelekeza katika maeneo yanayosababisha ukuaji wa uchumi ili kuongeza mapato ya serikali.

Wazee wa Afrika Mashariki

Aliagiza wizara kufanya utaratibu wa kuwalipa haraka wazee hao kwa kuwa limekuwa suala la muda mrefu.

1 comment:

  1. Kazi ya uwaziri ni pamoja na kumshauri raisi. Si vema raisi kupewa taarifa hii baada ya kutembelea wizara. Ilibidi tangu mapungufu haya yaanze kujitokeza, yangepelekwa kwenye baraza la mawaziri ili kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi mapema. Kama ilikuwa inajulikana kwa raisi tayari, basi hii si taarifa ya kumpatia raisi baada ya kutembelea wizara zake. TUWAJIBIKE KWA MAKINI NA UADILIFU KATIKA DHAMANA TULIZOPEWA.

    ReplyDelete